Breaking News

WIZARA YA MAMBO YA NDANI YA NCHI YAWATAKA MAAFISA WATENDAJI KATA KUJIRIDHISHA NA VIKUNDI VYA JAMII KATIKA MAENEO YAO


NA. Wizara ya Mambo ya ndani, Dar
Mwakilishi wa Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Ndani Nchi ambaye ni Mkurugenzi wa Utawala na Usimamizi wa Rasilimaliwatu, Miriam Mmbaga amefungua mafunzo ya kuwajengea uwezo kuhusu  masuala ya usajili na usimamizi wa jumuiya za kiraia kwa maafisa watendaji kata wa Jiji la Dar es Salaam  leo tarehe 15 Machi, 2024, katika ukumbi wa Arnatoglo Jijini Dar es Salaam.

Akizungumza kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Mmbaga amesema lengo la mafunzo hayo ni kujenga uwezo na uelewa wa pamoja  katika masuala yanayohusu usajili na usimamizi wa jumuiya za Kiraia na athari zinazotokana na uwepo wa uendeshaji wa jumuiya zisizozingatia Sheria na Taratibu za Nchi.

Bi, Mmbaga alitoa rai kwa watendaji hao kusimamia  na kuvifuatilia vikundi vya kijamii vinavyofanya shughuli mbalimbali katika Kata zao,  ili kuhakikisha vinafuata Sheria na Taratibu  zilizowekwa na Nchi yetu  pamoja  na kufahamu shughuli wanazozifanya.

Aliendelea kusema baada ya mafunzo haya tunaweza kuwa chachu ya mabadiliko na kuwa vinara katika usajili wa vikundi vya kijamii maana anayelinda Nchi ni mwananchi mwenyewe. "Kwa upande wa Mamlaka ya Serikali za Mitaa tutabaki salama, Nchi yetu ikiwa salama hata jitihada za Rais wetu Mhe.Dkt. Samia Suluhu Hassan zitazidi kusonga mbele" Alisema

Kwa upande wake Msajili wa Jumuiya za Kiraia, Emmanuel Kihampa alisema kusajili vikundi hivyo ni  kuiwezesha Serikali kutambua vikundi vilivyopo na kuvifikia kwa urahisi ili kutambua shughuli zinazoendelea katika vikundi ahli hii itasaiaia kulinda mila na desturi za  Nchi yetu.

Naye Husna Nondo Mwakilishi wa Watendaji Kata Mkoa wa Dar es Salaam alishukuru Wizara kwa mafunzo ya kuimarisha waliyopatiwa na kuahidi kufuatilia kwa ukaribu hatua zote za usajili wa vikundi hivyo "Tunataka kufanyiwa mafunzo haya mara kwa mara kwa kuwa  yatatuongezea ufanisi na uzalendo kwa taifa zima"