JESHI LA POLISI KUENDELEA KUTOA ELIMU NAMNA YA KUJIEPUSHA NA UTAPELI WA MITANDAO
Jeshi la polisi nchini limesema litaendelea kutoa elimu kwa wananchi kuhusu namna ya kijiepusha na utapeli na mikopo ya mitandani.
Akiwasilisha mada katika kongamano la waandishi wa mitandao ya kijamii nchini Msemaji wa Jeshi la Polisi, Naibu Kamishna wa Polisi (DCP) David Misime amesema kutokana na kukua kwa sayansi na teknolojia duniani changamoto kubwa imekuwa ni namna bora ya kuzuia na kuepusha wananchi na matukio hayo.
"Dunia nzima kumekuwepo na changamoto kubwa ya kuweza kuzuia matukio mbalimbali hususani utapeli na mikopo kwa njia ya mtandao hivyo jeshi la polisi kwa kutambua hilo limejikita zaidi katika kutoa elimu kwa wananchi juu ya jambo hilo" Alisema Misime.
Alisema pamoja na jitihada zinazochukuliwa na wadau wengine ikiwepo mamlaka ya mawasiliano nchini bado kuna haja kuwepo kwa ushirikiano kati ya wadau mbalimbali hususani wanahabari wa mitandao ya kijamii nchini kujikita kutoa elimu kwa wananchi juu ya matumizi sahihi ya mitandao.





