Breaking News

CUF YAITAKA SERIKALI KULIPA UMUHIMU SUALA LA WATU KUTEKWA, KUPOTEA NA KUAWA

Na Neema Mpaka - Chama Cha Wananchi (CUF) kimeiomba Serikali kulichukulia kwa uzito mkubwa suala la utekaji, kupotea na kuawa kwa watu katika mazingira ya kutatanisha.

Rai hiyo imetolewa leo Mei 29, 2025, jijini Dar es Salaam na Mwenyekiti wa Taifa wa chama hicho, Profesa Ibrahim Lipumba, wakati akifungua mkutano wa siku mbili wa Baraza la Uongozi la Taifa la CUF.

"Tupo kwenye kikao hiki huku nchi yetu ikikabiliwa na majaribu makubwa. Kuna malalamiko mengi kuhusu watu wanaodaiwa kutekwa, na hili ni suala zito kwa taifa letu," alisema Prof. Lipumba.

Akaongeza: “Hivi karibuni, Mchungaji Askofu Gwajima alisema ana orodha ya watu 83 waliopotea, baadhi yao wamepoteza maisha na wengine hawajulikani walipo. Hili ni jambo kubwa sana kwa nchi yetu.”

Profesa Lipumba alieleza kuwa suala la utekaji ndani ya CUF si jambo geni, akitoa mfano wa tukio la mwaka 2017 ambapo Diwani wa Viti Maalum wa CUF, Bi. Ziada Salum Nongwa, aliyekuwa akiishi Maporoni, Halmashauri ya Kibiti, alikamatwa na watu wanaodhaniwa kuwa askari usiku akiwa na mtoto wa mwezi mmoja, na hadi sasa hajulikani alipo
"Ziada alikamatwa, akawekwa kwenye mtumbwi kuelekea visiwa vya Kibiti na tangu siku hiyo hajawahi kuonekana. Mume wake alitufahamisha, nasi tukawa sehemu ya jitihada za kumtafuta, hata barua iliandikwa kwa Waziri Mkuu, lakini hadi leo hajapatikana," alisema.

Prof. Lipumba alisema kuwa kitendo cha watu kupotea au kuchukuliwa bila kufuata taratibu kinakiuka ibara ya 8, 14 na 15 za Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania zinazolinda haki za binadamu na ustawi wa wananchi.

Alisisitiza kuwa kutokana na malalamiko haya, Serikali ina wajibu wa kutoa msimamo na kuyachunguza kwa kina, huku akimhimiza Mchungaji Gwajima kuwasilisha rasmi orodha na taarifa alizonazo kwa vyombo vya dola ili vifanye uchunguzi huru na kutoa taarifa kwa umma.

Aidha, Prof. Lipumba aligusia matukio ya watu waliokamatwa baada ya kufika kusikiliza kesi ya Mheshimiwa Tundu Lissu na madai kwamba baadhi yao walihusishwa na vitendo visivyofaa.

"Mimi binafsi nimesikitishwa na kauli ya Mbunge wa Pandani, Bi. Mariam, aliyoitoa bungeni kana kwamba anashabikia watu kuteswa na kuumizwa. Tunapozungumzia haki sawa kwa wote, maana yake ni kwamba watu wasifanyiwe matendo mabaya. Mbunge huyo alikuwa mdogo mwaka 2001, lakini wakati huo visiwa vya Pemba vilipitia mateso makubwa," alisema.
Prof. Lipumba alisema CUF haiwezi kushabikia mateso au unyanyasaji wa raia wowote kwani sera zake ni kuheshimu haki za binadamu na kusimamia usawa kwa wananchi wote.

KUHUSU UCHAGUZI MKUU NA TUME HURU YA UCHAGUZI

Akizungumzia maandalizi ya Uchaguzi Mkuu ujao, Prof. Lipumba alisema vyama vya siasa vilitegemea uchaguzi huo kusimamiwa vizuri kutokana na mazungumzo ndani ya Baraza la Vyama vya Siasa na matarajio ya kupatikana kwa Tume Huru ya Uchaguzi (INEC), lakini matarajio hayo hayajatimia.

Hata hivyo, alibainisha kuwa kuna mambo yanayoweza kuboreshwa, akisisitiza umuhimu wa daftari la kudumu la wapiga kura kupatikana kwa vyama husika.

"Mwaka 2005 tulipata nakala ya daftari la kudumu la wapiga kura, lakini mwaka 2020 hatukupata. Pia kuna dosari zinazoashiria kuwepo kwa kura feki wakati wa uchaguzi. Safari hii hatutaki kuona hilo likijirudia," alisema.