Breaking News

ACT WAZALENDO YALAANI UNYAYASAJI WA RAIA WA AFRIKA MASHARIKI NCHINI



Chama cha ACT Wazalendo kinapinga na kulaani vikali matukio ya uvunjifu wa haki za binadamu, unyanyasaji wa kijinsia, na ukiukwaji wa mkataba wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, unaofanywa na mamlaka za Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Mnamo Mei 19, 2025, Kiongozi wa Chama cha Ukombozi wa Watu (People’s Liberation Party - PLP) kutoka Kenya, Mwanasheria Ndg. Martha Karua, pamoja na Jaji wa zamani wa Mahakama ya Juu ya Kenya, Jaji Willy Mutunga, walizuiwa kwa muda mrefu katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere na hatimaye kurejeshwa nchini kwao bila kutolewa kwa maelezo rasmi.

Katika siku hiyo hiyo, wanaharakati wengine kutoka nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki walikamatwa, kuwekwa kizuizini kwa zaidi ya siku tatu, kuteswa, na kurejeshwa makwao wakiwa na majeraha na maumivu. Miongoni mwao ni Ndg. Agatha Atuhaire kutoka Uganda, aliyepatikana karibu na mpaka wa Mtukula, na Ndg. Boniface Mwangi kutoka Kenya, aliyepatikana eneo la Kaunti ya Kilifi karibu na mpaka wa Tanzania na Kenya baada ya kushikiliwa kwa muda nchini Tanzania. Wanaharakati hawa wametoa ushuhuda kuhusu ukatili walioupitia wakiwa mikononi mwa vyombo vya dola vya Tanzania.

Katika taarifa mbalimbali zinaonyesha kuwa mwanajumuiya na Raia wa Uganda Ndg. Agather Atuhaire amenyanyaswa kingono na kupewa mateso makali akiwa kizuizini nchini Tanzania, taarifa zinaonesha kuwa Mwanahabari na mwanaharakati huyu alibakwa na kufanyiwa unyanyasaji mkubwa, jambo hili hatutarajii kufanywa chini ya Utawala wa Rais mwanamke, wakati huu ni wakati ambao tulitarajia mwanamke atalindwa kwa wivu mkubwa, heshima yake itarudi na kuzingatiwa lakini badala yake ndio wakati ambao matukio ya ukatili yanashamiri zaidi.

Matukio haya yanatia doa heshima ya kihistoria ya Tanzania kama taifa lililowahi kuwa kimbilio la wapigania uhuru, na kuchochea umoja wa bara la Afrika kwa kuwasha Mwenge wa Uhuru na kuusimika katika kilele cha Mlima Kilimanjaro Umulike na kuangaza kuleta matumaini palipo na kukata tamaa, Upendo palipo na Uadui na heshima palipo na chuki.

ACT Wazalendo inasikitishwa na kauli ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania aliyoitoa wakati wa uzinduzi wa Sera ya Mambo ya Nje (Toleo la 2024), ambapo alielekeza vyombo vya ulinzi na usalama pamoja na Wizara ya Mambo ya Nje kudhibiti wanaharakati wa Afrika Mashariki kuingia nchini, akiwataja kuwa ni “watovu wa adabu.” Kauli hii ni kinyume na Tamko la Sera ya Mambo ya Nje ibara ya 34 na 35 inayosisitiza ushirikiano wa kikanda na mtangamano.

Vilevile, tumefedheheshwa na kauli zisizo na utu zilizotolewa na baadhi ya Wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wakati wa mjadala wa bajeti ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, ambazo zinakiuka Katiba na Kanuni za Kudumu za Bunge. Kauli hizi zimeungwa mkono hadharani na Waziri wa Mambo ya Ndani, Ndg. Innocent Bashungwa, ambaye alieleza kuwa maoni hayo ya Wabunge yameviimarisha vyombo vya ulinzi na usalama.

Mwenendo huu unavunja kwa dhahiri Mkataba wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, hususan kipengele kinachotoa haki ya raia wa nchi wanachama kusafiri, kuishi na kufanya kazi katika nchi yoyote ya Jumuiya bila ubaguzi.

Matukio haya yameharibu heshima ya Tanzania na taasisi zake kama Serikali na Bunge, na yanaweka doa katika historia ya taifa letu ndani ya Afrika na dunia.

ACT Wazalendo inaitaka Serikali ya Tanzania pamoja na Jumuiya ya Afrika Mashariki kuchukua hatua zifuatazo;

1. Tunapinga vitendo vyote vya ukatili wa kijinsia dhidi ya raia, 

2. Jumuiya ya Afrika Mashariki iunde chombo huru cha uchunguzi kuhusu matukio haya ya ukiukwaji wa haki za binadamu dhidi ya raia wa Kenya na Uganda waliokuwa nchini Tanzania.

3. Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki atoe maelezo ya kina kuhusu sababu za kukamatwa, kuzuiliwa, kuteswa na kurejeshwa kwa raia hao wa Afrika Mashariki.

4. Wabunge waliotoa kauli za matusi na dharau dhidi ya wanaharakati hao wafikishwe mbele ya Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge, kwa mujibu wa maelekezo ya Spika wa Bunge, ikiwa kweli kauli hizo si msimamo rasmi wa Bunge. Hii ni pamoja na Ndg. Tauhida Gallos (Mb) na Ndg. Maryam Omar Said (Mb).

ACT Wazalendo tunatoa wito kwa Serikali ya Tanzania kuheshimu misingi ya utu, haki za binadamu na ushirikiano wa kikanda matukio ya Ukatili na unyanyasaji wa wananchi hayakubaliki na yanapaswa kuachwa maramoja.

Imetolewa na
Ndg. Janeth Joel Rithe
Waziri kivuli wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum.
ACT Wazalendo, Dar es salaam.
Mei, 29, 2025