RAIS SAMIA AOMBELEZA KIFO CHA CHARLES HILLARY
Nimepokea kwa masikitiko taarifa ya kifo cha Bw. Charles Hilary, Mkurugenzi wa Idara ya Mawasiliano Ikulu Zanzibar kilichotokea leo Mei 11, 2025.
Ninatoa pole kwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mheshimiwa Dkt. Hussein Mwinyi, familia, ndugu, jamaa na marafiki na wadau wote wa sekta ya habari nchini kwa msiba huu.
Ndugu Charles Hilary atakumbukwa kwa mchango wake adhimu wa zaidi ya miaka 40 katika kukuza sekta ya habari nchini tangu akiwa redioni hadi kwenye televisheni, pamoja na unasihi kwa wanahabari wachanga.
Namuomba Mwenyezi Mungu aijaalie familia yake uvumilivu na subra katika kipindi hiki kigumu, na ailaze roho ya mpendwa wetu mahala pema.
Hakika sote ni wa Mwenyezi Mungu, na kwake tutarejea.
Hii hapa historia yake katika utangazaji
Alikuwa Mkurugenzi wa ldara ya Mawasiliano Ikulu ya Zanzibar na Msemaji Mkuu wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Charles Hillary (66) amefariki dunia alfajiri ya leo Mei 11, 2025
Amefanya kazi Redio Tanzania mwaka 1981 hadi 1994 alipojiunga na Radio One Stereo. Mwaka 2003 alijiunga na Radio Deusch Welle (DW) nchini Ujerumani, na miaka mitatu baadaye alijiunga na BBC akiwa Idhaa ya Kiswahili. Mwaka 2015 aliamua kurejea nchini na kujiunga Azam Media. Desemba 30, 2021 aliteuliwa kuwa Mkurugenzi wa Idara ya Mawasiliano – Ikulu Zanzibar




