Breaking News

RASMI: HUDUMA ZA WIZARA YA MADINI KUPATIKANA MAKAO MAKUU MTUMBA

# Waziri Mavunde Atimiza Ahadi Kwa Kamati ya Nishati na Madini

Dodoma, Mei 15, 2025 – Waziri wa Madini, Mhe. Anthony Mavunde, ametangaza kuwa kuanzia leo huduma zote za Wizara ya Madini zitaanza kutolewa rasmi katika jengo jipya la Makao Makuu ya Wizara hiyo, lililopo eneo la Mtumba katika Mji wa Serikali, kufuatia kukamilika kwa ujenzi wa jengo hilo.

Akizungumza na Menejimenti ya Wizara, taasisi zilizo chini yake, na watumishi wote, Mhe. Mavunde ameipongeza Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kuwezesha kukamilika kwa jengo hilo la kisasa.
Ameeleza kuwa awali huduma za Wizara zilikuwa zikitolewa katika maeneo mbalimbali, jambo lililosababisha usumbufu kwa wadau. Hata hivyo, sasa huduma hizo zitapatikana mahali pamoja, hatua inayolenga kuongeza ufanisi na kurahisisha upatikanaji wa huduma kwa wananchi.

Akizungumza kabla ya Waziri, Naibu Waziri wa Madini, Dkt. Steven Kiruswa, aliishukuru Serikali kwa kufanikisha ujenzi huo pamoja na miundombinu yote inayohitajika kwa utendaji bora wa kazi. Alisema hatua hiyo itaongeza tija na kuleta matokeo chanya kwa Sekta ya madini.
Kwa upande wake, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara, Bw. Msafiri Mbibo, aliwapongeza watumishi wa Wizara kwa kuendelea kufanya kazi kwa bidii licha ya changamoto zilizokuwepo wakati wa ujenzi wa Makao Makuu hayo mapya.

Kuhamia kwa Wizara katika jengo hilo pia ni utekelezaji wa ahadi aliyoitoa Waziri Mavunde kwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini wakati wa ziara ya ukaguzi wa maendeleo ya ujenzi huo tarehe 20 Machi, 2025.

Jengo hilo limejengwa na Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) kwa gharama ya Shilingi bilioni 22.8, chini ya usimamizi wa Wakala wa Majengo Tanzania (TBA).