Breaking News

DPC YAPONGEZA JAB KUONGEZA MUDA USAJILI WA WAANDISHI WA HABARI

Dar es Salaam, Juni 23, 2025 – Klabu ya Waandishi wa Habari Mkoa wa Dar es Salaam (DAR-PC) imepongeza hatua ya Bodi ya Ithibati kwa Waandishi wa Habari (JAB) ya kuongeza muda wa usajili wa waandishi wa habari hadi Juni 28, 2025.

Uamuzi huo umetokana na ombi lililotolewa na wanachama wa DAR-PC kupitia Mkutano Mkuu uliofanyika Juni 21, 2025, ambapo walimwomba Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Mipango na Uwekezaji, Prof. Kitila Mkumbo kuwasilisha hoja hiyo kwa Waziri wa Habari, Utamaduni na Michezo, Prof. Paramagamba Kabudi. Serikali imeitikia wito huo kama sehemu ya usikivu wake kwa wadau wake.

Akizungumza kwa niaba ya klabu, Mwenyekiti wa DAR-PC, Bakari Kimwanga amesema kuwa wanapokea kwa mikono miwili hatua hiyo ya kuongeza muda, huku akiwasihi waandishi wote wenye sifa zinazostahili kuhakikisha wanatumia muda huo wa nyongeza kujisajili kupitia JAB.

"Tunatoa wito kwa waandishi wa habari kote nchini, hususan wale wa Dar es Salaam na hata kutoka mikoa mingine, kuhakikisha wanajisajili kwa mujibu wa sheria ili kuendelea kufanya kazi zao kwa ufanisi na kwa mujibu wa taratibu," alisema Kimwanga.

DAR-PC imeendelea kuhimiza ushirikiano kati ya serikali na wanahabari ili kukuza sekta ya habari kwa maslahi ya taifa.