ANTHONY ISHIKA MGHAMBA (AIM) ATANGAZA KUGOMBEA UBUNGE SAME MAGHARIBI KUPITIA ACT-WAZALENDO
Na mwandishi wetu - Anthony Ishika Mghamba, anayejulikana kwa kifupi kama AIM, ametangaza nia yake ya kugombea ubunge wa Jimbo la Same Magharibi kupitia Chama cha ACT-Wazalendo katika uchaguzi mkuu ujao.
Akizungumza na waandishi wa habari, Mghamba amesema endapo atapewa ridhaa na chama chake pamoja na wananchi wa Same Magharibi, atatumia kaulimbiu isemayo: "Uongozi Shirikishi, Uchumi Imara, Miundombinu Bora na Huduma Bora za Jamii."
Mghamba amesema kuwa dhamira yake kuu ni kushirikiana na wananchi katika kupanga na kutekeleza miradi ya maendeleo, kukuza uchumi wa wananchi wa kawaida, kuboresha miundombinu ya barabara, maji na umeme, pamoja na kuhakikisha upatikanaji wa huduma bora za afya, elimu na ustawi wa jamii.
"Ninaamini kuwa kwa ushirikiano wa kweli kati ya kiongozi na wananchi, tunaweza kujenga Jimbo la Same Magharibi lenye maendeleo jumuishi na endelevu," alisisitiza Mghamba.
Kwa sasa, Anthony Ishika Mghamba anaendelea na mikutano ya kusikiliza maoni ya wananchi kabla ya mchakato rasmi wa uteuzi ndani ya chama kuanza.




