CRDB Bima YABORESHA HUDUMA KWA WAKULIMA NA WAFUGAJI NCHINI
Dar es Salaam — Wakulima na wafugaji nchini wataanza kunufaika moja kwa moja na huduma za bima kupitia mawakala wa CRDB waliopo kote nchini, hatua inayolenga kuboresha maisha ya Watanzania kwa ujumla na kuwawezesha kujiamini katika shughuli zao za kila siku za kujitafutia kipato.
Akizungumza na vyombo vya habari leo katika Maonesho ya 49 ya Biashara ya Kimataifa yanayoendelea katika Viwanja vya Sabasaba, Afisa Mauzo Bima wa Kanda ya Pwani, Justina Byalugaba, amesema CRDB Bima imeongeza ubunifu na ufanisi wa huduma zake kwa lengo la kumgusa kila Mtanzania.
Byalugaba amesema kuwa mwaka huu, CRDB Bima imeboresha huduma zake maradufu ili ziendane na mahitaji na matarajio ya wateja. Miongoni mwa maboresho hayo ni uharakishaji wa malipo ya madai kwa wateja walioathirika na ajali ndogo. Endapo gharama ya hasara ni chini ya Shilingi Milioni 3, mteja hatalazimika kuwasilisha nyaraka za polisi, na malipo yatashughulikiwa ndani ya saa 24 bila usumbufu au ucheleweshaji.
"CRDB Bima tumejipanga vizuri. Mteja atakapopata tatizo la aina hiyo, tutahakikisha ndani ya saa 24 anapata fidia yake na anaweza kuendelea na shughuli zake kama kawaida," alisisitiza Byalugaba.
Katika hatua nyingine ya kuendeleza sekta ya mifugo, CRDB Bima imezindua bima ya mifugo inayolenga kuwapa kinga wafugaji dhidi ya majanga mbalimbali kama ajali, kuanguka, kupigwa shoti ya umeme, kifo kutokana na moto, moshi, radi, mafuriko, maporomoko ya ardhi, kimbunga, hadi mashambulizi ya nyoka na wadudu.
Bima hiyo pia inalinda dhidi ya magonjwa hatari ya mifugo ikiwemo kichaa cha mbuzi, homa ya milipuko (Anthrax), matatizo ya uzazi, uchinjaji wa dharura, wizi, pamoja na magonjwa sugu yanayosababisha vifo kama saratani na mastitis.
"Ahadi yetu ni kuhakikisha tunawalinda wafugaji wa Tanzania, kusaidia usalama wa chakula kwa taifa na kuunga mkono ukuaji wa sekta ya kilimo na ufugaji," amesema Byalugaba.
Mbali na sekta ya mifugo, CRDB Bima pia imeendelea kuboresha huduma kwa wakulima kupitia mpango wa Kijani Bima, unaolenga kuwasaidia wakulima wakubwa na wadogo kupata kinga ya kifedha dhidi ya majanga ya kilimo.
Kwa kuimarisha huduma hizi, CRDB Bima inaonyesha dhamira yake ya dhati ya kuwa mshirika wa kweli katika maendeleo ya kijamii na kiuchumi ya Watanzania.




