FCC YAWAHAKIKISHIA WAWEKEZAJI WA NDANI ULINZI WA KISHERIA
Dar es Salaam – Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Ushindani nchini (FCC), Bi. Hadija Juma Ngasongwa, amesema kuwa wawekezaji wa ndani wanalindwa na kusimamiwa na sheria madhubuti zinazolenga kuimarisha na kulinda biashara zao.
Akizungumza leo Jijini Dar es Salaam alipotembelea banda la Wizara ya Viwanda na Biashara katika Maonyesho ya 49 ya Biashara ya Kimataifa (maarufu kama Sabasaba), Bi. Ngasongwa alieleza kuwa FCC itaendelea kutekeleza maagizo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, katika kuhakikisha mazingira ya biashara yanaboreshwa na kuimarishwa kwa ustawi wa uchumi wa taifa.
"Lengo la kuanzishwa kwa Tume ya Ushindani ni kusimamia na kuhimarisha ufanyaji wa biashara nchini, kulinda walaji dhidi ya mienendo potofu ya kibiashara kati ya kampuni na kampuni, pamoja na kudhibiti bidhaa bandia," alisema Bi. Ngasongwa.
Aidha, aliongeza kuwa moja ya dhamira kuu ya tume hiyo ni kuhakikisha kuwa wawekezaji wa ndani wanatambua kuwa kuna sheria thabiti zinazolinda uwekezaji wao dhidi ya changamoto mbalimbali zinazoweza kujitokeza katika mazingira ya kibiashara.
Bi. Ngasongwa alitumia nafasi hiyo kuipongeza Serikali kwa kuweka mazingira rafiki kwa wawekezaji wa ndani, jambo ambalo limewawezesha kupata fursa mbalimbali za uwekezaji na biashara kwa ufanisi zaidi.
Akizungumzia ushiriki wa FCC katika maonyesho ya mwaka huu, alieleza kuwa ni fahari kubwa kwao kushiriki, na kuwaalika wananchi na wageni wa maonyesho kutembelea banda la Wizara ya Viwanda na Biashara ili kupata elimu na taarifa kuhusu sheria za ushindani na ulinzi wa walaji.
"Tuna zaidi ya makampuni 3000 yanayoshiriki kwenye banda la Wizara. Tunaamini mwekezaji mwenye mtaji mdogo anaweza kushirikiana na mwekezaji mwenye uwezo mkubwa ili kuimarisha biashara zao kwa pamoja," alisisitiza.
Aidha, Bi. Ngasongwa alikemea vikali biashara ya bidhaa bandia na kueleza kuwa ni kosa la jinai kujihusisha nazo. Alihimiza wananchi kufika kwenye banda la FCC ili kupata elimu juu ya namna ya kutambua bidhaa halisi dhidi ya bidhaa bandia kutoka kwa wataalamu waliopo.
Maonyesho ya Sabasaba yameendelea kuwa jukwaa muhimu kwa taasisi na makampuni mbalimbali nchini kuonyesha huduma na bidhaa, pamoja na kuhamasisha uwekezaji na ubunifu katika sekta ya viwanda na biashara.





