Breaking News

DKT. BUSANDA LUCAS BUSANDA ATANGAZA NIA YA KUGOMBEA UBUNGE JIMBO LA BUSANDA KUPITIA CCM

Busanda – Daktari wa binadamu, Dkt. Busanda Lucas Busanda, ametangaza rasmi nia yake ya kugombea ubunge wa Jimbo la Busanda kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Dkt. Busanda, ambaye ni mtaalamu wa afya na mwenye uzoefu wa miaka kadhaa katika sekta ya tiba, amesema ameamua kuingia kwenye siasa kwa lengo la kuwatumikia wananchi wa Busanda kwa moyo wa uzalendo na uadilifu. Akizungumza na wanahabari, Dkt. Busanda alisema kuwa anatambua changamoto zinazowakabili wananchi wa jimbo hilo, hususan katika sekta ya afya, elimu na miundombinu, na anaamini ana uwezo na maono ya kuzitatua kwa kushirikiana na serikali na wananchi.

“Ninakuja na ajenda ya maendeleo jumuishi. Uzoefu wangu katika sekta ya afya utanisaidia kushirikiana na mamlaka husika kuboresha huduma za afya, sambamba na kushughulikia mahitaji mengine muhimu kwa wananchi wa Busanda,” alisema Dkt. Busanda.

Wananchi kadhaa waliozungumza kuhusu nia hiyo wameonyesha matumaini na kumpongeza kwa hatua ya kujitokeza, wakisema jimbo linahitaji viongozi wenye uelewa wa changamoto halisi za jamii.

Mchakato wa kura za maoni ndani ya CCM unatarajiwa kuanza hivi karibuni, ambapo wanachama wa chama hicho watapata fursa ya kuchagua mgombea atakayewakilisha chama katika uchaguzi mkuu ujao.