Breaking News

MUINJA MAINGU ACHUKUA FOMU YA KUGOMBEA UBUNGE JIMBO LA MUSOMA VIJIJINI KUPITIA CCM

Mjumbe wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Kada Muinja Maingu, leo amechukua rasmi fomu ya kugombea ubunge wa Jimbo la Musoma Vijijini.

Akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kuchukua fomu hiyo, Maingu alisema kuwa amefanya tathmini ya kina na kujiridhisha kuwa anayo sifa na uwezo wa kulitumikia jimbo hilo kwa ufanisi.

“Nimeamua kugombea ubunge kwa kuwa ninauelewa wa kutosha kuhusu changamoto na mahitaji ya wananchi wa Musoma Vijijini. Ninaamini ninaweza kuwa sehemu ya suluhisho,” alisema Maingu.

Aliongeza kuwa uamuzi wake umetokana na dhamira ya dhati ya kuleta maendeleo ya kweli kwa wananchi wa jimbo hilo, akiahidi kuwa atashirikiana nao kwa karibu endapo atapata ridhaa ya kuwa mwakilishi wao bungeni.

Hatua ya Maingu imezidi kuongeza ushindani ndani ya CCM katika mchakato wa kuwapata wagombea wa nafasi hiyo kuelekea uchaguzi mkuu ujao.