Breaking News

PURA YAWAITA WAWEKEZAJI KUWEKEZA KWENYE NISHATI SAFI

Dar es Salaam, Julai 9, 2025 – Mamlaka ya Udhibiti Mkondo wa Juu wa Petroli (PURA) imetoa wito kwa wawekezaji wa ndani na nje ya nchi kuchangamkia fursa za kuwekeza katika sekta ya Nishati Safi, kufuatia kuwepo kwa mazingira bora ya uwekezaji, amani, utulivu na mikakati madhubuti ya maendeleo ya kiuchumi nchini.

Akizungumza na waandishi wa habari katika Maonesho ya 49 ya Biashara ya Kimataifa (Sabasaba) yanayoendelea jijini Dar es Salaam, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa PURA, Mhandisi Charles Sangweni, amesema kuwa mazingira wezeshi yaliyopo nchini yamechangia kwa kiasi kikubwa kuongezeka kwa ajira katika sekta ya uzalishaji wa mafuta na gesi kutoka asilimia 55 hadi 85.

"Tangu mwaka 2017 tumekuwa tukishiriki maonesho haya na mwaka huu tumeshuhudia mafanikio makubwa. Maonesho yameendeshwa kidijitali zaidi na tumepata fursa ya kujibu maswali mengi ya wananchi kuhusu nishati safi, na tunaamini wamepata elimu stahiki," amesema Mhandisi Sangweni.

Amesema kuwa tangu kuanzishwa kwa PURA, mamlaka hiyo ilikuwa na watumishi 45 tu, lakini sasa imeajiri watumishi 95, hatua ambayo ni mafanikio makubwa. Ameeleza kuwa mafanikio hayo yamechangiwa na uwekezaji mkubwa uliofanywa na serikali chini ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan.

"Uwekezaji wa serikali katika mamlaka hii umeleta mabadiliko makubwa, kuanzia mishahara hadi mazingira rafiki ya kufanyia kazi. Hili ni tukio la kutia moyo na tunawaalika wawekezaji kutumia fursa hii kuwekeza katika nishati safi nchini," aliongeza.

Mhandisi Sangweni pia amesema kuwa kati ya kampuni 10 zinazojihusisha na utafutaji wa mafuta na gesi nchini, sita ni za Kitanzania. Hii ni matokeo ya utekelezaji wa mkakati wa serikali wa kuimarisha elimu ya mafuta na gesi katika vyuo vya ndani, ambapo wahitimu wanaingia moja kwa moja kwenye soko la ajira.

Kuhusu miradi ya uzalishaji, amesema kuwa kwa sasa PURA iko kwenye maandalizi ya kuchimba visima vitatu vya gesi asilia mkoani Mtwara kuanzia Novemba mwaka huu. Visima hivyo vinatarajiwa kuongeza uzalishaji wa gesi kutoka kitalu cha Mnazi Bay kwa zaidi ya ujazo wa milioni 30 kwa siku, hatua ambayo itakuwa ni mafanikio makubwa kwa nchi.