Breaking News

DOYO HASSAN DOYO WA NLD AREJESHA FOMU ZA URAIS KWA UCHAGUZI MKUU MKUU 2025

Dodoma – Mgombea wa urais kupitia Chama cha National League for Democracy (NLD), ambaye pia ni Katibu Mkuu wa chama hicho, Mhe. Doyo Hassan Doyo, amerejesha rasmi fomu za uteuzi wa kugombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika Ofisi za Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) zilizopo Njedengwa, Dodoma.

Mhe. Doyo aliwasili katika ofisi hizo akiambatana na mgombea mwenza wake Bi. Chausiku Khatibu Mohamed, pamoja na viongozi waandamizi wa chama hicho. Fomu hizo zilikabidhiwa kwa mujibu wa matakwa ya kisheria na kupokelewa rasmi na Tume, hatua inayothibitisha uteuzi wao kuwania nafasi ya Rais na Makamu wa Rais katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025.

Akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya zoezi hilo, Mhe. Doyo alisema:

“Leo ni siku ya kihistoria kwa chama chetu na kwa Watanzania kwa ujumla. Tumechukua hatua hii kwa nia njema ya kuleta mabadiliko ya kweli na kulinda haki za kila Mtanzania. Tulichukua fomu na sasa tumerejesha fomu zetu huku tukikidhi vigezo vyote kwa mujibu wa sheria na kanuni za uchaguzi.”

Kwa mujibu wa taarifa ya chama hicho, NLD imeeleza kuwa ina imani thabiti na mgombea wake kutokana na maono, uzoefu na dhamira yake ya dhati ya kulitumikia taifa kwa misingi ya haki, uwazi na uadilifu.

Chama hicho pia kimetoa wito kwa wanachama wake na Watanzania kwa ujumla kushiriki kikamilifu katika hatua zote za uchaguzi kwa misingi ya amani, mshikamano, uzalendo na maendeleo ya taifa.