TAMWA YAWAPONGEZA WANAWAKE WALIOJITOKEZA KUWANIA UONGOZI UCHAGUZI MKUU
Dar es Salaam – Chama cha Wanahabari Wanawake Tanzania (TAMWA) kimewapongeza wanawake wote waliojitokeza kuwania nafasi za uongozi kuanzia udiwani, ubunge hadi urais katika Uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba 29, 2025.
Kwa mujibu wa takwimu za Ulingo Wanawake, jumla ya wanawake 231 walichukua fomu za ubunge kupitia CCM, ambapo 25 kati yao wameteuliwa kugombea, nane wakiwa ni wapya. Aidha, vyama mbalimbali vya siasa mwaka huu vimeongeza idadi ya wanawake walioteuliwa kuwa wagombea wenza katika nafasi ya urais na makamu wa rais.
Kwa mara ya kwanza katika historia ya chama tawala, CCM imemteua Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan kugombea urais, hatua ambayo TAMWA imeielezea kuwa ya kihistoria na inayoashiria mwelekeo mpya wa ushiriki wa wanawake katika uongozi wa juu nchini.
Mbali na Samia, wanawake wengine walioteuliwa kugombea nafasi ya urais ni pamoja na Mwajuma Noty Mirambo wa UMD aliyekuwa na mgombea mwenza Mashavu Alawi Haji. Wagombea wenza wanawake kutoka vyama vingine ni pamoja na Eveline Wilbard Munis (NCCR-Mageuzi), Husna Mohamed Abdallah (CUF), Aziza Haji Selemani (MAKINI), Amani Selemani Mzee (TLP), Chausiku Khatibu Mohamed (NLD), Sakia Mussa Debwa (SAU), Chuma Juma Abdallah na Devotha Minja (CHAUMA).
Akizungumza kupitia taarifa kwa vyombo vya habari, Mkurugenzi Mtendaji wa TAMWA, Dkt. Rose Reuben, alisema chama hicho kinatambua ujasiri wa wanawake waliothubutu kugombea licha ya changamoto mbalimbali wanazokabiliana nazo, ikiwemo mfumo dume na udhalilishaji, hasa kwenye mitandao ya kijamii.
Taarifa za Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) zinaonyesha hadi Februari 2024, wanawake walikuwa asilimia 37.4 ya wabunge (148 kati ya 392), wengi wakiwa kupitia viti maalum. Ripoti za Aprili na Julai 2024 pia zinaonyesha kuwa wanawake walikuwa asilimia 37.5 ya mawaziri nchini.
TAMWA imeeleza kuwa licha ya mafanikio haya, bado kuna changamoto kubwa katika kuhakikisha wanawake wanashiriki kikamilifu kwenye siasa na uongozi. Chama hicho kimeendelea kutoa elimu kupitia warsha, makongamano na vyombo vya habari ili kuhakikisha wanawake wanashiriki katika mazingira yenye usawa na usalama.
“Uwepo wa wanawake katika uongozi ni muhimu kwa maendeleo ya taifa kwani huongeza uwajibikaji, usawa wa kijinsia na kulinda maslahi ya makundi yote hususan wanawake na watoto,” ilisema sehemu ya taarifa hiyo.
Aidha, TAMWA imetoa wito wa kampeni safi, zenye staha na jumuishi, ikisisitiza kuwa itafuatilia mwenendo wa kampeni na kuripoti ukiukwaji wowote wa kanuni za uchaguzi ili hatua za kisheria zichukuliwe.