Breaking News

JOSIAH GIRLS’ SECONDARY SCHOOL YAADHIMISHA MIAKA 15 YA MAFANIKIO

Josiah Girls’ Secondary School ya Bukoba imeadhimisha miaka 15 tangu kuanzishwa kwake mwaka 2010, ikiwa taasisi ya elimu inayojivunia kutoa malezi bora na elimu yenye maadili kwa wasichana ndani na nje ya mkoa wa Kagera.

Sherehe hizo ziliambatana na Ibada Kuu ya Shukrani iliyoongozwa na viongozi wa dini, serikali na jamii.
Askofu Dkt. Alex Malasusa wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) alisisitiza umuhimu wa kumtegemea Mungu katika safari ya elimu, huku Askofu mstaafu Methodius Kilaini akipongeza mshikamano na uthubutu wa uongozi wa shule. Vilevile, Askofu Dkt. Abednego Keshomshahara alitambua mafanikio makubwa ya kitaaluma yaliyopatikana katika kipindi cha miaka 15.

Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Bukoba, Mhe. Erasto Siima, aliahidi kuendeleza ushirikiano kati ya serikali na shule hiyo, hususan katika kuboresha miundombinu na mazingira ya kujifunzia.
Katika kipindi cha miaka 15, Josiah Girls’ Secondary School imeendelea kushirikiana na wadau wa elimu, wazazi na jamii kwa ujumla huku ikikuza vipaji, kuimarisha maadili, na kuhamasisha matumizi ya teknolojia na akili bandia (AI) kwa kizazi kipya cha wasichana.

Kaulimbiu ya maadhimisho hayo ilikuwa “Ndoto Yangu, Upeo Wangu.”