NLD YATANGAZA MAJIMBO 23 WANACHAMA WAKE WALIOCHUKUA FOMU ZA UBUNGE 2025
Dar es Salaam, Agosti 19, 2025 – Chama cha National League for Democracy (NLD) kimetangaza majimbo 23 nchini ambako wanachama wake wamejitokeza kuchukua fomu za kuomba kuteuliwa kugombea ubunge katika Uchaguzi Mkuu wa 2025.
Kwa mujibu wa taarifa kwa vyombo vya habari iliyosainiwa na Mkurugenzi wa Mipango na Uchaguzi Taifa wa NLD, Don Waziri Mnyamani, kufikia saa 6 mchana leo, wanachama katika majimbo hayo tayari walikuwa wamechukua fomu, hatua inayodaiwa kuashiria hamasa kubwa ya ushiriki wa wanachama wa chama hicho kwenye mchakato wa kidemokrasia.
Majimbo ambayo wanachama wa NLD tayari wamechukua fomu ni: Mvumi, Segerea, Iramba Magharibi, Dodoma Mjini, Babati Mjini, Bunda Mjini, Sumve, Kwimba, Kondoa Mjini, Singida Mjini, Arusha Mjini, Ukerewe, Nyamagana, Buchosa, Sengerema, Ilongero, Korogwe Mjini, Ukonga, Arumeru Magharibi, Arumeru Mashariki, Kawe, Kinondoni na Kibaha.
Akizungumzia hatua hiyo, Mnyamani alisema chama kitaendelea kuhamasisha wanachama na wananchi kushiriki kikamilifu katika mchakato wa uchaguzi.
“NLD inaamini ushiriki wa wananchi katika mchakato wa uchaguzi ni msingi wa kuimarisha demokrasia na kujenga taifa lenye mshikamano wa kweli wa kidemokrasia,” alisema.