UNFPA YASISITIZA USHIRIKIANO WA VYOMBO VYA HABARI KATIKA KUFANIKISHA TDV 2050
Dar es Salaam, Agosti 19, 2025 – Shirika la Umoja wa Mataifa la Idadi ya Watu (UNFPA) limewataka wanahabari nchini kushirikiana kikamilifu na Serikali ya Tanzania katika kufanikisha Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050 (TDV 2050).
Wito huo umetolewa na Naibu Mwakilishi na Kaimu Mkuu wa UNFPA nchini Tanzania, Bi. Melissa McNeil-Barrett, wakati wa warsha maalum kwa waandishi wa habari iliyolenga kujadili nafasi ya vyombo vya habari katika utekelezaji wa dira hiyo ya kitaifa.
Akizungumza kwenye warsha hiyo, Bi. McNeil-Barrett alisema TDV 2050 inalenga kuboresha huduma za afya, elimu na kuongeza ushiriki wa vijana katika maamuzi yanayohusu maisha yao. Alibainisha kuwa dira hiyo imejengwa katika misingi ya usawa, ubunifu, maendeleo ya rasilimali watu na utunzaji wa mazingira.
“Utekelezaji wa TDV 2050 unahitaji ushiriki wa wananchi wote. Vyombo vya habari vina wajibu mkubwa wa kutoa elimu na kuhamasisha jamii kuelewa na kushiriki katika kufanikisha malengo haya,” alisema Bi. McNeil-Barrett.
Aidha, alisisitiza kuwa mafanikio ya dira hiyo yatatokana na mshikamano wa kitaifa, ambapo kila sekta ikiwemo vyombo vya habari itachukua jukumu lake ipasavyo katika kuelimisha na kushirikisha wananchi.
Warsha hiyo imeandaliwa kwa ushirikiano wa UNFPA, Serikali kupitia Tume ya Mipango, pamoja na wadau mbalimbali wa maendeleo.