Breaking News

ADC YAZINDUA KAMPENI DAR KWA KISHINDO, MVUNGI ATAJA VIPAUMBELE VYAKE JIMBO LA KAWE

Mgombea wa urais kupitia Chama cha ADC, Wilson Elias akinadi sera zake katika mkutano wa chama hicho uliofanyika leo Jumamosi, Septemba 27, 2025 katika viwanja vya Tanganyika Peckars jijini Dar es Salaam.
Mgombea ubunge wa Jimbo la Kawe kupitia ADC, Hassan Mvungi akizungumza katika Uzinduzi wa kampeni hizo ambapo ametaja vipaumbele vyake leo Jumamosi, Septemba 27, 2025 katika viwanja vya Tanganyika Peckars jijini Dar es Salaam

Dar es salaam - Chama cha Alliance for Democratic Change (ADC) leo, Septemba 27, 2025, kimezindua rasmi kampeni zake katika viwanja vya Tanganyika Packer, Kawe, jijini Dar es Salaam, kwa ajili ya kuomba kura za urais, ubunge na udiwani.

Mgombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia ADC, Wilson Elias, akihutubia mamia ya wananchi waliohudhuria uzinduzi huo, alisema chama chake kimejipanga kuhakikisha kinawaletea maendeleo wananchi kwa kuweka mazingira wezeshi, hususan kwa wajasiriamali.

“Sisi ADC, mkituchagua na kutupa ridhaa ya kuunda serikali, tutahakikisha kuwa rasilimali zilizopo zinatumika kwa manufaa ya taifa na wananchi wote ili kuwakwamua kiuchumi na kuwaletea maendeleo ya kweli,” alisema Elias.

Kwa upande wake, mgombea ubunge wa Jimbo la Kawe kupitia ADC, Hassan Mvungi, aliwataka wananchi wa jimbo hilo kujitokeza kwa wingi Oktoba 29 na kuwachagua wagombea wa chama hicho kuanzia ngazi ya urais, ubunge hadi udiwani.

Mvungi alisema dhamira ya ADC ni kuwaletea wananchi huduma bora za kijamii ikiwemo maji, afya na miundombinu, ambazo amedai zimekuwa zikisuasua katika kipindi cha uongozi wa chama tawala.

Aidha, alitaja baadhi ya vipaumbele vyake kuwa ni:

Kutoa mikopo nafuu kwa vijana na kuondoa mikopo kandamizi.

Kujenga stendi za daladala katika kata za Kawe na Msasani, na kuboresha stendi ya Bunju.

Kuboresha barabara, kujenga machinjio ya kisasa Tegeta, na kujenga soko la Kawe kwa kiwango cha kimataifa pamoja na masoko ya Msasani na Bunju.

Kuhakikisha elimu bure inatekelezwa kwa viwango na kuondoa michango holela mashuleni.

Uzinduzi huo ulihudhuriwa na viongozi mbalimbali wa chama hicho na kuambatana na shamrashamra za kisiasa zilizoashiria kuanza kwa kampeni rasmi za ADC jijini Dar es Salaam.