Breaking News

AHADI ZA KAMPENI YA MGOMBEA URAIS WA CCM, DKT. SAMIA SULUHU HASSAN TUNDUMA - SONGWE

Mgombea wa Urais wa CCM, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, ameendelea kuchanja mbunga kusaka kura za kuomba dhamana ya utumishi kwa watanzania katika nafasi ya Urais. Ambapo jana tarehe 3 Agosti mwaka 2025 amefanya mikutano mikubwa ya kampeni katika majimbo ya Tunduma na Vwawa mkoani Songwe. Mhe Dkt. Akiwa Tunduma aliwashukuru wananchi kwa kujitokeza kwa wingi kwenye mkutano wa kampeni, na hasa vijana kwa mshikamano wao mkubwa. Aliwaeleza wananchi kuwa safari ya maendeleo itaendelea kwa kasi zaidi endapo watamchagua tena kuongoza nchi katika kipindi cha 2025-2030.

Aliahidi kuendeleza sekta za elimu, afya, maji na umeme kwa kuongeza shule, kuendeleza sera ya elimu bila ada, na kuongeza mikopo kwa wanafunzi ili vijana wote wapate fursa ya masomo. Aidha, aliahidi kujenga vyuo vya VETA katika mkoa wa Songwe, ili vijana wapate ujuzi na kujiandaa kwa ajira na kujiajiri. Kuhusu afya, alisisitiza kuwa hospitali mpya, vituo vya afya na zahanati zaidi vitajengwa ili wananchi wapate huduma karibu na makazi yao.

Kwa upande wa maji, Dkt. Samia aliahidi kumaliza miradi mikubwa ya maji, kwa lengo la kuhakikisha kila Mtanzania anapata maji safi na salama, kufikia asilimia zaidi ya 90 upatikanaji vijijini na mijini. Vilevile.. alisema kuwa kila kaya itapatiwa huduma ya umeme na kuongeza kuwa ahadi yake ya Bima ya Afya kwa Wote tayari imeanza kufanyiwa majaribio, ambapo serikali itabeba gharama za matibabu kwa wale wasio na uwezo.
Akizungumzia miundombinu, alieleza kuwa maboresho makubwa yaliyofanyika Bandari ya Dar es Salaam yameongeza tani ya mizigo inayopita Tunduma, na sasa serikali imeanza kukarabati barabara kuu ya TANZAM, Aliahidi kukamilisha kipande cha Igawa-Tunduma na Songwe-Tunduma (km 75) na kuendelea na vipande vilivyosalia, sambamba na kuimarisha reli ya TAZARA ili iwe ya kisasa zaidi na iweze kubeba mizigo kwa haraka.

Aidha Dkt. Sarnia, aliahidi kukamilisha ujenzi wa bandari kavu kubwa ya ekari 1.800 eneo la Katenjele, kata ya Mpemba, ili kuondoa msongamano wa malori barabarani. Pia, barabara mbadala zitajengwa, sambamba na maegesho ya kisasa na mizani mpya, Amesisitiza pia kwamba atahakikisha nyaraka za mizigo zinachakatwa mapema kabla ya kufika mpakani ili kupunguza muda wa kusubiri. Dkt. Samia alisema atazungumza na Zambia kuhakikisha nao, kupitia mamlaka ya mapato, wanafanya kazi saa 24 ili wananchi wapate huduma kwa haraka.
Mhe Dkt. Samia Kuhusu nishati, amewaomba wananchi wa Tunduma kumpa kura nyingi za ndiyo ili akamilishe mradi wa umeme mkubwa wa KV 730 kutoka Iringa, Njombe hadi Songwe, ambapo KV 430 zitatumika Songwe na kV 300 zitaelekezwa Zambia. Alibainisha kuwa mazungumzo ya kuuza umeme yameanza na kwa wakati huo huo serikali yake Itaendelea kuhamasisha matumizi ya nishati safi majumbani ili kuboresha maisha ya wananchi,

 VWAWA

Akiwa katika jimbo la Vwawa Mhe. Dkt. Samia Suluhu aliwahutubia wananchi katika mkutano uliofanyika Vwawa. Katika mkutano huo aliahidi kukamilisha ujenzi wa barabara muhimu ya Kamsamba na kuhakikisha wilaya zote zinaunganishwa na barabara za lami hadi makao makuu ya mkoa.

Kuhusu sekta ya kilimo, Dkt. Samia alieleza kuwa changamoto ya upatikanaji wa mbolea iko mbioni kutatuliwa kwani mbolea ya kupandia tumbaku na mazao mengine tayari imeingia na ipo kwenye hatua ya kusambazwa, Alitumia nafasi hiyo kupongeza wakulima kwa mafanikio makubwa, akibainisha kuwa Tanzania imeshika nafasi ya pili barani Afrika kwa uzalishaji wa chakula, hususan mahindi, na kwamba taifa lina kiwango cha 128% cha utoshelevu wa chakula. Alisema mafanikio haya yamechochewa na mpango wa ruzuku ya pembejeo unaotekelezwa na serikali ya CCM.
Kuhusu nishati, alibainisha kuwa umeme si changamoto kubwa tena Songwe, lakini ataendelea na mkakati wa kujenga njia mpya ya kusafirisha umeme yenye uwezo wa kV 730. Kati ya hizo, kV 430 zitatumika katika mikoa ya kusini, huku kV 300 zikielekezwa Zambia kama sehemu ya mpango wa biashara ya nishati. Alisisitiza pia umuhimu wa nishati safi na akaahidi kuialika sekta binafsi kushiriki katika kujenga vituo vya kusambaza nishati hiyo.

Kwa upande wa vijana, aliahidi kuendeleza fursa kwao kupitia mikopo ya elimu na ujenzi wa vyuo vya VETA katika mkoa wa Songwe. Amesema kuwa ada na gharama za mafunzo hayo zitabebwa na serikali, ili kuhakikisha vijana wote wenye nia na uwezo wa kusoma wanapata nafasi ya kupata ujuzi na hatimaye ajira.