CHAUMMA: TUKISHIKA DOLA, WANANCHI VIJIJINI KUJENGEWA NYUMBA ZA KISASA
Mgombea mwenza Urais wa Chama cha Ukombozi wa Umma (Chaumma) Devotha Minja amesema kutokana na wananchi wengi kuishi vijijini chama hicho kikishika dola wananchi hao watajengewe nyumba za kisasa na watalipa kwa miaka 50.
Amesema haiwezekani wananchi kuendelea kuishi katika nyumba za tembe wakati Serikali inaweza kujenga nyumba na kuwakopesha wananchi, waishi maisha bora.
Msingi wa kauli ya Devotha umejikita katika takwimu za Ofisi ya Taifa ya Takwimu Tanzania (NBS) ambazo zimebainisha takribani asilimia 60 hadi 70 ya Watanzania wanaishi vijijinii
Devotha ametoa kauli katika kata ya Pahi Jimbo la Kondoa Vijini katika muendelezo wa kampeni ya chama hicho kusaka imani kwa wananchi ili Oktoba 29,2025 kwenye uchaguzi mkuu chama hicho kipate ridhaa.
"Nyumba za tembe zipo au hazipo kwani kuna Watanzania wanapenda kuishi maisha duni tupeni Chaumma,ilani yetu inaelekeza kwa kuwa wananchi wengi wanaishi vijijini na makazi yao ni duni na kipato chao ni kidogo,tukiingia madarakani tunataka maisha bora kwa kila Mtanzania"amesema.
Devotha amesema Chaumma itaweka mkakati bora wa makazi ambao mwananchi atajengewa nyumba na kulipa kidogo kidogo Serikalini kwa miaka 50.
Utekelezaji wa mkakati huo ni kupitia sekta binafsi ambayo Serikali itaibinafsisha sekta ya umma inayotoa huduma ya makazi kwa wananchi.