Breaking News

CHINI YA RAIS SAMIA MRADI WA NICKEL KABANGA KUTOA AJIRA 3,800

Mradi wa uchimbaji na usindikaji wa nickel wa Kabanga, unaomilikiwa kwa asilimia 84 na kampuni ya Lifezone Metals na asilimia 16 na Serikali ya Tanzania, umepokea ufadhili wa dola za Marekani milioni 60 kutoka Taurus Mining Finance Fund kwa ajili ya kuanza kazi za awali na ujenzi wa miundombinu.

Kwa mujibu wa mpango wa utekelezaji, mradi huo unatarajiwa kuzalisha jumla ya tani milioni 52.2 za ore kwa kipindi cha miaka 18, zikiwa na wastani wa asilimia 1.98 ya nickel, asilimia 0.27 ya shaba na asilimia 0.15 ya kobati. Aidha, kiwanda cha usindikaji kitakachojengwa kitazalisha hadi tani milioni 3.4 za concentrate kwa mwaka, kwa gharama ya wastani wa dola 3.36 kwa pauni moja ya nickel.

Chini ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan, mradi huo unatarajiwa kuzalisha zaidi ya tani 30,000 za nickel kwa mwaka. Vilevile, mradi utatoa ajira za moja kwa moja takribani 800 na zaidi ya ajira zisizo za moja kwa moja 3,000, hatua itakayochochea ukuaji wa Sekta ya Madini na kuongeza mchango wake katika pato la Taifa.

Mradi wa Kabanga unatarajiwa pia kuongeza thamani ya rasilimali za madini nchini na kutoa fursa kwa wachimbaji wadogo kushiriki katika mnyororo wa thamani wa madini hayo.