Breaking News

CHINI YA RAIS SAMIA: UJENZI WA SGR KIPANDE CHA MANYONI – SINGIDA MJINI KUANZA

Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania chini ya Rais Samia Suluhu Hassan inatarajia kuanza maandalizi ya ujenzi wa kipande cha Reli ya Kisasa (SGR) kutoka Manyoni hadi Singida mjini chenye urefu wa kilometa 164, sambamba na njia ya reli ya zamani ya MGR.

Kwa mujibu wa taarifa kutoka Wizara ya Ujenzi, eneo hili ni tambarare na halihitaji madaraja marefu wala milima mikubwa, hivyo gharama za ujenzi zinakadiriwa kufikia kati ya shilingi trilioni 2.0 hadi 2.8, sawa na dola za Kimarekani milioni 820 hadi 1,150. Mradi huu unatarajiwa kukamilika ndani ya kipindi cha miaka 3 hadi 4.

Aidha, wakati wa ujenzi zaidi ya wananchi 1,300 hadi 2,000 wanatarajiwa kupata ajira za moja kwa moja huku zaidi ya watu 4,000 wakipata ajira zisizo za moja kwa moja kupitia huduma mbalimbali.

Kukamilika kwa mradi huu kutarahisisha usafirishaji wa abiria na mizigo, kupunguza gharama za usafirishaji kwa zaidi ya asilimia 30 hadi 40, na kufungua fursa kubwa kwa wakulima, wafugaji na wafanyabiashara wa Mkoa wa Singida. Mazao ya kipaumbele ni pamoja na alizeti, ufuta, vitunguu pamoja na mifugo, hatua ambayo itachochea ukuaji wa uchumi wa mkoa na taifa kwa ujumla.