DKT. LEYNA ATOA WITO KWA WADAU KUUNGA MKONO JITIHADA ZA KUBORESHA LISHE NCHINI
Dar es salam - Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Chakula na Lishe, Dkt. Germana Leyna, ametoa wito kwa wadau wa masuala ya lishe nchini kuendelea kuunga mkono juhudi za kupambana na changamoto zinazohusiana na lishe.
Akizungumza katika mahojiano maalum kupitia kipindi cha Jambo Tanzania kinachorushwa na Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) jijini Dar es Salaam, kuelekea Mkutano Mkuu wa 11 wa Wadau wa Masuala ya Lishe, Dkt. Leyna amesema Tanzania imepiga hatua kubwa katika kukabiliana na changamoto hizo kupitia mikakati madhubuti ya serikali.
Amesema serikali imeendelea kutoa elimu kwa umma ili kuongeza uelewa wa jamii kuhusu lishe bora, lengo likiwa ni kuwa na taifa lenye watu wenye afya bora. Aidha, amewataka wadau kuunganisha nguvu katika kupambana na changamoto za lishe nchini.
Dkt. Leyna ameongeza kuwa serikali imejipanga kuwafikia wazalishaji hususan wakulima ili kuwapatia elimu ya lishe bora na umuhimu wa kutunza chakula cha matumizi ya nyumbani badala ya kuuza chote.
Ametumia fursa hiyo kuwataka wadau wa masuala ya lishe kuendelea kujitokeza na kuchangia juhudi za serikali katika kukuza lishe bora kwa wananchi.






