CUF YAITUHUMU CCM NEWALA MTWARA CHAKUSANYA KADI ZA MPIGA KURA KINYUME NA SHERIA
Mgombea Ubunge wa Jimbo la Newala Vijijini (CUF), na Mwenyekiti wa CUF wilaya ya Newala na Mkurugenzi wa Mambo ya Nje, Sera, Bunge na Utafiti CUF Taifa. Mneke Jafari Saidi, akifafanua jambo kwa waandishi wa habari makao makuu ya chama hicho jijini dar es salaam
Mkurugenzi wa Habari na Uenezi CUF Taifa ambaye pia ni mgombea ubunge Jimbo la Kilwa Kaskazini, Eng. Mohamed Ngulangwa akizungumza na waandishi wa habari kuhusu Chama cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Newala kufanya zoezi haramu la ukusanyaji wa kadi za wapiga kura kinyume na sheria za uchaguzi makao makuu ya chama hicho jijini dar es salaam
Dar es salaam – Mgombea Ubunge wa Jimbo la Newala Vijijini kupitia Chama cha Wananchi (CUF), Mneke Jafari Saidi, ameituhumu Chama cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Newala kwa kufanya zoezi haramu la ukusanyaji wa kadi za wapiga kura kinyume na sheria za uchaguzi.
Akizungumza na wanahabari, Mneke ambaye pia ni Mwenyekiti wa CUF Wilaya ya Newala na Mkurugenzi wa Mambo ya Nje, Sera, Bunge na Utafiti wa CUF Taifa, alisema viongozi wa CCM wamekuwa wakikusanya kadi za wapiga kura vijijini kwa muda wa zaidi ya mwezi mmoja kwa madai ya kuzihakiki.
“Nyuma ya kadi ya mpiga kura imeandikwa wazi kuwa ni mali ya Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi na hairuhusiwi kutolewa kwa mtu mwingine asiyehusika. CCM kwa makusudi wamechukua jukumu la Tume ya Uchaguzi,” alisema Mneke .
Ameeleza kuwa kitendo hicho kinakiuka sheria za uchaguzi na kinyume na falsafa ya maridhiano ya 4Rs ya Rais Samia Suluhu Hassan, ambaye ameahidi Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025 utakuwa huru na haki.
Mneke alisema tayari amewasilisha malalamiko yake kwa Jeshi la Polisi, Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa na Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC), lakini hatua madhubuti hazijachukuliwa hadi sasa.
Tarehe 20 Septemba 2025, polisi walikamata viongozi wawili wa CCM katika Kijiji cha Nakahako wakiwa na kadi kadhaa za wapiga kura walizokusanya. Hata hivyo, Saidi alidai watuhumiwa hao waliachiwa bila kufikishwa mahakamani huku kadi zikiendelea kushikiliwa na polisi.
“Kitendo hiki si tu kwamba kinahatarisha uchaguzi huru na haki, bali pia kinapandikiza mbegu za chuki na uhasama miongoni mwa wananchi,” alisema Mneke.
CUF imeitaka Tume ya Uchaguzi kueleza uhalali wa CCM kufanya uhakiki wa kadi za wapiga kura na Jeshi la Polisi kutoa majibu ni kwa nini halichukui hatua za kisheria dhidi ya wanaohusika.
Aidha, Mneke amemtaka Katibu Mkuu wa CCM kuwaelekeza viongozi wa chama hicho kuacha mara moja ukusanyaji huo na kuwarejeshea wananchi kadi zao. Pia amemuomba Rais Samia kuchukua hatua dhidi ya wanasiasa na watendaji wanaohujumu dhamira yake ya kuhakikisha uchaguzi huru na haki.
Amewataka wananchi waendelee kuwa watulivu, kuepuka kuchokozeka kisiasa na kujitokeza kwa wingi kushiriki uchaguzi Oktoba 29.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Habari na Uenezi CUF Taifa ambaye pia ni mgombea ubunge wa Jimbo la Kilwa Kaskazini, Eng. Mohamed Ngulangwa, alimtaka Katibu Mkuu wa CCM kukomesha hujuma hizo akisema zinakinzana na kauli za Mwenyekiti wa CCM kuhusu uchaguzi wa amani na haki.
“Hatuko tayari kuona yaliyotokea katika kampeni za uchaguzi wa mwaka 2020 yakijirudia tena, kwani yanapingana na falsafa ya Rais Samia ya kuhakikisha uchaguzi huru na haki,” alisema Eng. Ngulangwa.







