DKT. SAMIA AENDELEA NA KAMPENI KANDA YA KATI, ATOA AHADI KUBWA ZA MAENDELEO
BAHI, DODOMA – Mgombea urais kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dkt. Samia Suluhu Hassan, ameendelea na kampeni zake za kuomba ridhaa ya wananchi kwa muhula wa pili kwa kishindo kikubwa, akivutia maelfu ya wananchi kwenye mikutano ya hadhara mkoani Dodoma na Singida.
Katika mkutano uliofanyika Bahi, Dodoma, Dkt. Samia aliambatana na viongozi kadhaa wa kitaifa akiwemo Naibu Katibu Mkuu wa CCM, Ndg. John Mongela, Katibu wa Itikadi na Uenezi, Ndg. Kenan Kihongosi, na Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Dodoma, Ndg. Adam Kimbisa.
Akiwahutubia wananchi, Dkt. Samia alieleza vipaumbele vya serikali yake endapo CCM itapewa tena ridhaa.
Elimu
Amesisitiza serikali itaendelea kutoa elimu bure kwa shule za umma na kujenga mabweni ya wasichana wilayani Bahi. Aidha, kwa mkoa wa Singida ameahidi kujenga vyuo vya VETA wilayani Manyoni na Ikungi, pamoja na shule mpya na miundombinu ya elimu Singida Mjini.
Maji
Katika sekta ya maji, amewaahidi wananchi wa Bahi na Manyoni kufanikisha mradi wa gridi ya maji ya taifa kutoka Ziwa Victoria, kwa matumizi ya nyumbani, kilimo na ufugaji. Kwa Ikungi, amesema kutakuwa na usambazaji wa awali katika maeneo yenye changamoto kubwa wakati mradi mkubwa unasubiriwa.
SGR na Miundombinu
Amesema mradi wa reli ya kisasa (SGR) awamu ya pili na tatu utanufaisha moja kwa moja wakazi wa Bahi na Itigi (Singida), huku akiahidi kulipa fidia kwa wananchi waliopisha mradi huo. Ameeleza pia ujenzi wa barabara kuu na za vijijini utaendelezwa, ikiwemo Daraja la Sanza (Manyoni), barabara ya Noranga–Itigi, na uboreshaji wa barabara za Ikungi na Singida Mjini.
Kilimo na Viwanda
Dkt. Samia ameahidi kuanzisha mashamba makubwa wilayani Bahi ili kuinua vipato vya vijana, kuendelea kutoa ruzuku za pembejeo Ikungi, na kujenga maghala ya mazao. Aidha, amesisitiza mkakati wa ujenzi wa kongani za viwanda Bahi, Ikungi na Singida Mjini, lengo likiwa kuongeza thamani ya mazao na ajira kwa vijana.
Umeme na Nishati
Kwa upande wa nishati, amesema serikali yake imefikisha umeme vijijini kwa kiwango kikubwa, na kinachofuata ni kumalizia vitongoji vilivyosalia. Pia ametangaza kuwa mradi wa gridi imara na uzalishaji wa umeme wa jua utatekelezwa Singida kuanzia mwaka 2026.
Afya
Amesema serikali itaendeleza miradi ya hospitali na vituo vya afya katika wilaya zote, huku akiahidi kutekeleza sheria ya Bima ya Afya kwa Wote ndani ya siku 100 za kwanza za uongozi mpya. Katika Singida Mjini, ameeleza mafanikio yaliyopatikana, ikiwemo hospitali nne, vituo vya afya 22 na zahanati 63 mpya.
DKT. BASHIRU: SAMIA NI KIONGOZI WA UTULIVU NA UJASIRI
Akihutubia katika moja ya mikutano hiyo, Katibu Mkuu mstaafu wa CCM na Mratibu wa Kampeni Kanda ya Kati, Dkt. Bashiru Ally, aliainisha sababu kuu zinazomfanya Dkt. Samia Suluhu Hassan kuwa chaguo sahihi kwa watanzania.
Miongoni mwa hoja zake ni:
1. Ushuhuda wa kihistoria – Ujasiri alioonesha baada ya kifo cha Rais Magufuli na wakati wa changamoto ya UVIKO-19.
2. Falsafa ya umoja na usawa – Kusimamia amani, mshikamano wa kitaifa na usawa wa kijinsia.
3. Uongozi wa wanawake – Kuwapa nafasi nyingi wanawake katika uongozi bila upendeleo bali kwa ujasiri na uwezo.
4. Elimu – Mageuzi makubwa ya sera ya elimu bure na uwekezaji katika miundombinu ya elimu.
“Dkt. Samia hapaniki. Ana utulivu na uvumilivu wa hali ya juu. Ameonyesha ujasiri na uthabiti wa kulivusha taifa kwenye vipindi vigumu, jambo linalomfanya kustahili muhula mwingine wa uongozi,” alisema Dkt. Bashiru.
Kwa ujumla, ziara za kampeni za Dkt. Samia Kanda ya Kati zimeonyesha mapokezi makubwa kutoka kwa wananchi wa Dodoma na Singida, huku CCM ikinadi utekelezaji wa miradi mikubwa ya kitaifa na ahadi za maendeleo ya kijamii na kiuchumi.