Breaking News

DKT. SAMIA AENDELEA NA KAMPENI MAKAMBAKO, MUFINDI, MAFINGA NA IRINGA VIJIJINI

Makambako, Iringa – Mgombea wa urais kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dkt. Samia Suluhu Hassan, ameendelea na ziara zake za kampeni kuelekea uchaguzi mkuu wa 2025 kwa kufanya mikutano katika maeneo mbalimbali ya mikoa ya Njombe na Iringa. Katika mikutano hiyo iliyofanyika Septemba 6, 2025, aliahidi kuendeleza kasi ya maendeleo kwa kuzingatia sekta kuu ikiwemo elimu, afya, kilimo, viwanda na miundombinu ya barabara.

Makambako

Akihutubia wananchi wa Makambako, Dkt. Samia alisema amekuja kuomba kura kutokana na mambo mawili makuu: mafanikio yaliyopatikana katika kipindi cha uongozi uliopita wa CCM, na mipango iliyopangwa kutekelezwa kupitia Ilani ya 2025–2030.

Alibainisha kuwa serikali inafungua vituo vinane vya kununua mahindi mkoani Njombe ili kuwawezesha wakulima kupata masoko ya uhakika. Pia aliahidi kuanzishwa kwa One Stop Center Makambako ili kuufanya mji huo kuwa kitovu cha biashara, pamoja na kuangalia uwezekano wa kuanzisha bandari kavu.

Kuhusu elimu ya juu, alisema maandalizi ya ujenzi wa Chuo cha Mwalimu Nyerere yamekamilika na serikali itagharamia ujenzi huo. Aliahidi pia kuwa ombi la Makambako kupandishwa hadhi kuwa wilaya litazingatiwa katika awamu ijayo.

Mufindi (Nyororo)

Katika mkutano uliofanyika Mufindi, Dkt. Samia aliwaeleza wananchi kuwa kipaumbele kikubwa ni kuimarisha miundombinu ya barabara, ikiwemo barabara ya Nyororo–Mtwango yenye urefu wa km 40.4 ambayo ujenzi wake unaendelea, pamoja na barabara ya Igowelo–Kasanga–Nyigo yenye urefu wa km 54.5.

Aidha, alisema ombi la mashine ya X-Ray kwa hospitali ya wilaya linafanyiwa kazi. Kuhusu kiwanda cha Mgololo, alibainisha kuwa serikali inafanyia tathmini upya madai mapya yaliyowasilishwa ili malipo halali yalipwe. Pia alieleza kuwa kiwanda cha chai cha Mufindi kimepata mkopo wa shilingi bilioni 2.7 kutoka benki za Tanzania kwa ajili ya kufufua uzalishaji.
Alisisitiza kuwa serikali itaendelea kusogeza karibu huduma za kijamii ikiwemo elimu, afya, maji na umeme, huku akiahidi mikopo ya wanafunzi wa vyuo vikuu kuendelea kupatikana.

Mafinga

Katika mkutano uliofanyika Mafinga, Dkt. Samia aliwashukuru wananchi kwa kujitokeza kwa wingi na kusema kuwa umati huo ni ishara ya imani kwa CCM. Aliahidi kuendeleza miradi ya maendeleo katika sekta za elimu, afya, maji na umeme, sambamba na kuboresha miundombinu ya barabara.

Kuhusu viwanda, alisema serikali itaweka kongani za viwanda kulingana na mazao ya kilimo na misitu ili kufikia masoko ya kimataifa. Aliahidi pia kuendelea kutoa ruzuku za pembejeo na mbegu bora kwa wakulima, pamoja na chanjo kwa mifugo.
Kwa upande wa masoko, alisema vituo vya kununua mazao vitafunguliwa Njombe, Iringa na Mbeya, huku akiahidi kujengwa kwa stand mpya ya kimataifa Mafinga.

Kalenga – Iringa Vijijini

Akizungumza na wananchi wa Kalenga, Dkt. Samia alisema CCM inalenga kujenga taifa lenye uchumi jumuishi unaojitegemea. Alisisitiza kuwa maendeleo yanayogusa maisha ya wananchi wa kawaida ndiyo msingi wa taifa imara.

Alibainisha kuwa serikali imetekeleza miradi ya umeme vijijini, maji safi, pamoja na ujenzi wa shule mpya. Kuhusu barabara, alisema bajeti imetengwa kwa ajili ya mradi wa Makumbusho–Kalenga, na tayari mtandao wa barabara za lami umeongezwa kwa km 32 huku km 191 za changarawe na madaraja 34 yakiwa yamejengwa.

Aidha, aliahidi kujengwa kwa daraja katika kijiji cha Maperamengi na Kitwiru–Isakalilo, sambamba na uchimbaji wa mabwawa mapya kwenye awamu ijayo ya mpango wa maendeleo.

Dkt. Samia alihitimisha mikutano yake kwa kuwataka wananchi wa Iringa na Njombe kuendelea kuiamini CCM na kuchagua chama hicho ili kuendeleza kasi ya maendeleo katika miaka mitano ijayo.