Breaking News

MAADHIMISHO YA SIKU YA FARU DUNIANI YAFANA KARATU

Karatu — Maafisa na Askari wa Hifadhi ya Ngorongoro kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi Karatu, wadau wa uhifadhi, sekta ya utalii na wananchi wa mji wa Karatu wameadhimisha Siku ya Faru Duniani kwa mbio za kilomita tano zilizolenga kuhamasisha jamii kuhusu umuhimu wa kulinda mnyama Faru.

Maadhimisho ya mwaka huu yamebeba kaulimbiu isemayo “Tuhakikishe aina tano za Faru waliopo duniani wanaishi”, yakisisitiza wajibu wa dunia nzima kuhakikisha vizazi vijavyo vinaendelea kushuhudia uwepo wa mnyama huyo adimu.
Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro imeandaa shughuli mbalimbali ikiwemo utoaji wa elimu kwa jamii kuhusu uhifadhi wa Faru, kampeni za utunzaji wa mazingira, maonesho ya uhifadhi na michezo ya kijamii, yote yakiwa na lengo la kuongeza uelewa na ushiriki wa wananchi katika kulinda urithi huu wa kipekee.

Kwa mujibu wa viongozi wa uhifadhi, Faru ni miongoni mwa wanyama walio hatarini kutoweka kutokana na ujangili na uharibifu wa makazi yao, hivyo mshikamano wa jamii na wadau wote ni nyenzo muhimu katika vita ya kuhifadhi rasilimali za asili za Taifa.