Breaking News

MAADILI YA KI AFRIKA YAHIMIZWA, WAZAZI WATAKIWA KUWAELIMISHA WATOTO

Na Woinde Shizza, Arusha - Mkurugenzi wa Tanzania Platforms Network, Edward Malecela, amewataka wazazi nchini kutoacha jukumu la kuwaelimisha watoto wao kuhusu maadili ya Kiafrika na madhara ya tabia zisizo sahihi zinazoletwa na utandawazi kupitia simu na mitandao ya kijamii.

Akizungumza kwenye mahafali ya darasa la saba katika shule ya Oola Pre and Primary School iliyopo kata ya Esilale, wilayani Monduli, Malecela alisema wazazi hawapaswi kuogopa kuwaeleza ukweli watoto wao kwa hofu ya mila za zamani.

“Kwa mfano baba anaweza kumshauri binti yake, vivyo hivyo mama akamshauri mtoto wa kiume. Ni lazima wazazi tuwe wazi, tuwafundishe watoto maadili pasipo kuwaficha ili wajue faida na hasara za mambo wanayokutana nayo,” alisema Malecela.

Aliongeza kuwa mbali na kutoa elimu ya maadili, taasisi yake pia inajihusisha na ufadhili wa masomo kwa wanafunzi kutoka familia za kifugaji, kutoa elimu juu ya mazingira, haki za binadamu na afya ya uzazi. Pia, alisema taasisi hiyo inashirikiana na volunteers kutoka mataifa mbalimbali wanaosaidia katika masuala ya kijamii, afya na magonjwa yasiyoambukizwa kama kisukari na saratani.

Alisisitiza umuhimu wa elimu ya ujasiriamali na haki za wanawake wakati wa semina maalumu kwa kina mama iliyofanyika sambamba na mahafali ya darasa la saba katika shule ya Mchipuo wa Kiingereza, Oola Pre and Primary School, iliyopo kata ya Esilale, wilayani Monduli.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa shule hiyo, Samweli Oola, alisema shule hiyo imehitimisha darasa la saba kwa mara ya saba tangu ianzishwe, ambapo jumla ya wanafunzi 49 wamehitimu mwaka huu.

Alibainisha kuwa shule hiyo imekuwa ikiwasaidia wazazi wa jamii ya kifugaji kwa ada nafuu, ikiwemo mfumo wa kulipia kwa mifugo au mazao.

“Tunawaalika wazazi kuwaleta watoto wao hapa. Hawatajutia, maana tunafundisha elimu bora na maadili mema ya Kiafrika yatakayowasaidia katika maisha yao ya baadaye,” alisema Oola.

Mmoja wa wahitimu, Methew Laisheri, alieleza shukrani zake akisema awali aliacha shule kwa ajili ya kufuga mifugo, lakini ushawishi wa walimu ulimrudisha shuleni na sasa amehitimu akiahidi kuendelea na masomo zaidi.

Mgeni rasmi katika mahafali hayo, mgombea ubunge wa Monduli, Joseph Isack maarufu ‘Kadogoo’, aliwapongeza walimu na uongozi wa shule hiyo kwa kutoa elimu bora, huku akiahidi kuwa mlezi wa shule hiyo.

Aliwataka wananchi kuendelea kuiombea nchi kipindi cha kampeni na kujitokeza kwa wingi kupiga kura Oktoba 29, ili uchaguzi uwe wa amani na utulivu.