Breaking News

PBA YAPINGA ZUIO LA TLS KWA WANASHERIA KUTOA MSAADA WA KISHERIA

Dar es Salaam — Chama cha Mawakili wa Serikali (PBA) kimepinga vikali uamuzi wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS) kutoa maelekezo yanayowazuia wanasheria kutoa msaada wa kisheria kwa wananchi, kufuatia tukio la kushambuliwa kwa Wakili Deogratius Mahinyila na askari polisi Septemba 15, 2025 alipokuwa akifuatilia kesi ya Mwenyekiti wa CHADEMA, Tundu Lissu.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, Mwenyekiti wa PBA, Wakili Ado Mwasongwe, alisema chama hicho kimeona ni muhimu kutoa ufafanuzi wa kisheria na kikatiba ili kulinda maslahi ya taifa na haki za wananchi.

“TLS ni chama cha kitaaluma kilichoanzishwa kwa mujibu wa sheria. Kila wakili aliyeandikishwa ni mwanachama wake, wakiwemo mawakili wa Serikali na hata Mwanasheria Mkuu wa Serikali. Ni lazima tamko lolote la TLS liwe na weledi wa kisheria, si msukumo wa kiharakati,” alisema Wakili Mwasongwe.

Kwa mujibu wa PBA, hatua ya TLS ni kinyume cha Katiba na Sheria ya Msaada wa Kisheria, na inaleta hatari ya kunyima wananchi wa kipato cha chini haki yao ya msingi ya kupata msaada wa kisheria.

“Huduma za msaada wa kisheria si hiari wala hisani, bali ni jukumu la kisheria lililowekwa kwa mujibu wa Sheria ya Msaada wa Kisheria. Kila wakili anapaswa kutoa huduma hiyo kwa wote, wenye uwezo na wasio na uwezo,” aliongeza.

Amefafanua kuwa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (Ibara ya 13) inasisitiza usawa mbele ya sheria, huku Ibara ya 26 ikimtaka kila mtu kutii Katiba na sheria.

“Hatua ya TLS ya kuwanyima wananchi wa kipato cha chini msaada wa kisheria ni kitendo cha ubaguzi na kinyume cha Katiba,” alisisitiza.

Aidha, Mwasongwe alikumbusha kuwa nidhamu ya mawakili ipo chini ya Kamati ya Nidhamu ya Mawakili inayoongozwa na Jaji wa Mahakama Kuu, hivyo si jukumu la TLS pekee.

 “Tunashauri kwa heshima viongozi wa TLS kuzingatia wajibu wao wa kisheria na kitaaluma, na waache mara moja kuchagua sheria za kutii kulingana na maslahi yao binafsi,” alisema.

PBA imesisitiza kuwa itaendelea kutetea utawala wa sheria, kulinda maslahi ya taifa na kuhakikisha wananchi wote, hususan wenye kipato cha chini, wanapata huduma za kisheria bila ubaguzi.