Breaking News

RC CHALAMILA: MARUFUKU KUTUMIKA MABAUNSA KUTOA WATU MAENEO YENYE MIGOGORO

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Mhe. Albert Chalamila, amepiga marufuku matumizi ya mabaunsa katika kuwaondoa watu kwenye maeneo yenye migogoro ya ardhi na mali jijini Dar es Salaam.

Agizo hilo limetolewa leo, Septemba 24, alipofika katika nyumba yenye mgogoro iliyopo Msasani Beach, kufuatia tukio la Septemba 23 ambapo video zilionesha mabaunsa wakitumia nguvu kubwa kuwaondoa wapangaji wa nyumba hiyo, kitendo kilicholalamikiwa kuwa ni ukiukaji wa sheria na haki za binadamu.

RC Chalamila amesema kuanzia sasa madalali wa mahakama watapaswa kushirikiana na Jeshi la Polisi pekee katika utekelezaji wa shughuli hizo kwa kuwa polisi wana weledi wa kisheria na kijamii katika kusimamia masuala ya mgogoro.
Aidha, ameamuru nyumba hiyo, iliyoko kiwanja namba 891, kutotumika na upande wowote hadi mgogoro utakapomalizika. Amesema Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni ataongoza kamati ya wataalamu kutoka Jeshi la Polisi, Ofisi ya Kamishna wa Ardhi na taasisi nyingine husika ili kupitia mgogoro huo. Kamati hiyo imeagizwa kuripoti kwa RC Ijumaa, Septemba 26.

Mgogoro huo unahusisha Bi. Alice Paskali Haule, mjane wa marehemu Justis Lugaibula, na Bw. Muhamed Mustafa Yusufali. Bi. Alice ameeleza kuwa nyumba hiyo walinunua pamoja na marehemu mwaka 2008, na anadai Yusufali alipewa mkopo na mumewe badala ya kuuziwa nyumba hiyo.
Hata hivyo, mwakilishi wa Yusufali, Bi. Hajja Mungula, amesema nyumba hiyo ilinunuliwa na Yusufali mwaka 2011 kwa shilingi milioni 262, na kwamba Bi. Alice alitia dole gumba kwenye nyaraka za mauziano.

Kwa upande wake, Kamishna Msaidizi wa Ardhi mkoa wa Dar es Salaam, Bw. Shukrani Kyando, amesema nyaraka zilizopo zinaonesha umiliki upo kwa Yusufali. Naye Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Mhe. Saad Mtambule, amesisitiza changamoto ya matumizi ya mabaunsa wasio na weledi katika wilaya hiyo.