WAZIRI KOMBO ATUA JIJINI ARUSHA KUUNGANA NA MAWAZIRI WA MAMBO YA NJE WA JUMUIYA YA AFRIKA MASHARIKI KUSHIRIKI MKUTANO WA 35 WA BARAZA LA KISEKTA LA MAWAZIRI LA JUMUIYA HIYO.
Arusha - Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Mahmoud Thabit Kombo (Mb), amewasili Jijini Arusha na kuongoza Ujumbe wa Tanzania kwenye Mkutano wa 35 wa Baraza la Kisekta la Mawaziri wa Jumuiya ya Afrika Mashariki,
Mkutano huo unaofanyika katika ngazi tatu tofauti, umeanza rasmi tarehe 31 Agosti hadi tarehe 02 Septemba, 2025 kwa ngazi ya Wataalam, baada ya hapo ukaendelea kwa ngazi ya Makatibu Wakuu tarehe 03 hadi 04 Septemba, 2025 na hii leo unaingia katika awamu ya tatu ya ngazi ya Mawaziri, ambapo unatarajiwa kuchukua siku mbili, tarehe 05 hadi 06 Septemba, 2025.
Mawaziri wanaoshiriki mkutano huu ni Mawaziri wote wa Mambo ya Nje wanaoshughulikia masuala ya Jumuiya ya Afrika Mashariki kutoka nchi zote wanachama wa Jumuiya hiyo.
Baraza hili la Mawaziri la Kisekta la Jumjuiya, leo linapokea na kujadili taarifa mbalimbali zilizoanza kujadiliwa katika ngazi ya Wataalam na Makatibu Wakuu, zikiwemo taarifa za Utekelezaji wa Maamuzi na Maelekezo yaliyopita ya Baraza la Kisekta lililopita, Rasimu ya Mkakati wa Saba (7) wa Maendeleo ya Jumuiya ya Afrika Mashariki, Dira ya Jumuiya ya Afrika Mashariki ya Mwaka 2050, Mkakati wa Mageuzi ya Kidigitali wa Mwaka 2025 - 2030, Maandalizi ya Sera ya Lugha ya Jumuiya ya Afrika Mashariki pamoja na Kalenda ya Majukumu ya Jumuiya kwa kipindi cha mwezi Julai hadi Desemba, 2025 na hatua iliyofikiwa katika uondoaji wa vikwazo visivyo vya kiforodha Katika Jumuiya, na hatua iliyofikiwa katika masuala ya Kisiasa ya Nchi Wanachama wa Jumuiya hiyo ya Afrika Mashariki.
Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) ni Jumuiya ya nchi nane za Kanda ya Maziwa Makuu ya Afrika ikijumuisha Jamhuri ya Burundi, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Jamhuri ya Kenya, Jamhuri ya Rwanda, Jamhuri ya Shirikisho la Somalia, Jamhuri ya Sudan Kusini, Jamhuri ya Uganda na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Ikumbukwe kwamba lengo kuu la Jumuiya hii ni kukuza ushirikiano wa kikanda katika nyanja mbalimbali ikiwemo biashara, forodha na ushirikiano wa kisiasa. Jumuiya hii ilianzishwa awali mwaka 1967, lakini kutokana na tofauti za kisiasa ilivunjika mwaka 1977 kabla ya kufufuliwa rasmi mwaka 1999 kwa kutiwa Saini kwa Mkataba mpya.
Tangu kufufuliwa kwake, Jumuiya ya Afrika Mashariki imeanzisha hatua mbalimbali muhimu za ujumuishaji, ikiwa ni pamoja na kuanzishwa kwa Umoja wa Forodha mwaka 2005, Soko la Pamoja mwaka 2010, na juhudi zinazoendelea kuelekea Muungano wa Fedha. Jumuiya hiyo pia imekuwa ikifanya kazi ya kuoanisha sera katika sekta kama usafiri, afya, elimu, na nishati. Ikiwa na jumla ya watu wanaozidi milioni 300 na msisitizo wa pamoja juu ya maendeleo ya kikanda, EAC ina nafasi inayoongezeka katika masuala ya bara na inachukuliwa kama mfano wa ushirikiano wa kikanda barani Afrika.