Breaking News

WATAHIMIWA ZAIDI YA MILIONI 1 KUFANYA MTIHANI WA DARASA LA SABA KUANZIA KESHO

Dar es Salaam – Baraza la Mitihani la Taifa (NECTA) limetangaza kuanza kwa Mtihani wa Kumaliza Elimu ya Msingi, unaotarajiwa kufanyika kuanzia kesho Septemba 10 - 11 2025 nchini.

Akizungumza jijini Dar es Salaam, Katibu Mtendaji wa NECTA, Profesa Said Mohamed, amesema jumla ya watahiniwa 1,172,279 wamesajiliwa kufanya mtihani huo, ambapo wavulana ni 535,138 (asilimia 45.65) na wasichana ni 637,141 (asilimia 54.35).

“Kwa ujumla, asilimia 93.35 ya watahiniwa watafanya mtihani kwa lugha ya Kiswahili, huku asilimia 6.65 wakitarajiwa kutumia lugha ya Kiingereza, kulingana na lugha ya kujifunzia katika shule zao,” amesema Prof. Mohamed.

Aidha, Profesa Mohamed amebainisha kuwa watahiniwa 4,679 wenye mahitaji maalum wamesajiliwa kufanya mtihani huo. Kati yao, 92 ni wasioona, 1,551 ni wenye uoni hafifu, 1,079 wana uziwi, 448 wana ulemavu wa akili, na 1,509 wana ulemavu wa viungo.

“Maandalizi yote muhimu yamekamilika, yakiwemo usambazaji wa karatasi za mitihani, nyaraka muhimu, pamoja na maandalizi mahsusi kwa ajili ya watahiniwa wenye mahitaji maalum,” amesema.

Katika hatua nyingine, Baraza hilo limetoa wito kwa jamii, wamiliki wa shule, kamati za mitihani, na wasimamizi kuhakikisha kuwa mazingira ya mitihani yanakuwa salama, tulivu, na huru dhidi ya vitendo vya udanganyifu.

“Tunawasihi wamiliki wa shule na wakuu wa shule kutojihusisha kwa namna yoyote ile na usimamizi wa mitihani. Baraza halitasita kuchukua hatua, ikiwemo kufuta kituo cha mtihani, endapo kitabainika kuhatarisha uhalali wa mtihani,” amesisitiza Prof. Mohamed.

Mtihani wa kumaliza elimu ya msingi ni hatua muhimu katika safari ya elimu kwa wanafunzi nchini, na NECTA imesisitiza kuwa itaendelea kuchukua hatua madhubuti kulinda uadilifu wa mitihani hiyo.