CO-OPERATIVE BANK YASHIRIKI MAADHIMISHO YA USHIRIKA, YAJIPANGA KUSOGEZA HUDUMA ZA KIFEDHA KWA WANANCHI
Na Woinde Shizza, Arusha - Benki ya Ushirika Tanzania (Co-operative Bank) imedhamiria kuimarisha huduma zake za kifedha kwa wanachama wa vyama vya ushirika na wananchi kwa ujumla, huku ikibainisha mpango wa kufungua matawi zaidi nchini ili kuhakikisha huduma zake zinapatikana kwa urahisi.
Kauli hiyo imetolewa na Mkuu wa Kitengo cha Biashara wa benki hiyo, Yahya Jumamne Kiyabo, katika maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Vyama vya Ushirika yaliyofanyika kitaifa jijini Arusha ndani ya hoteli ya Lush Garden.
Kiyabo alisema benki hiyo, ambayo ilizinduliwa rasmi Aprili mwaka huu, tayari imefungua matawi manne katika mikoa ya Moshi, Dodoma, Tabora na Mtwara, na inaendelea na mpango wa kufungua matawi mengine ili kusogeza huduma karibu zaidi na wananchi.
“Benki ya Co-operative Bank imedhamiria kuwa benki ya wananchi kupitia vyama vya ushirika huduma tunazozitoa zinahusisha mikopo nafuu, akaunti za akiba, benki ya simu na elimu ya kifedha lengo letu likiwa ni kuhakikisha vyama vya ushirika vinakuwa chachu ya maendeleo ya taifa,” alisema.
Alisema benki hiyo ilizinduliwa kwa mtaji wa zaidi ya Shilingi bilioni 55, ambapo asilimia 51 ya hisa inamilikiwa na vyama vya ushirika kupitia shirikisho lao, huku asilimia 49 zikishikiliwa na wadau wengine
Alisema Kazi ya benki hiyo nipamoja kuhakikisha wananchi, hususani wakulima, wanawake na vijana, wanapata huduma za kifedha zenye urahisi, kuimarisha vyama vya ushirika kupitia mikopo na akiba, pamoja na kutumia teknolojia za kidijitali kusogeza huduma vijijini na mijini.
Aidha alibainisha kuwa benki hiyo inatoa huduma za mikopo ya kilimo, huduma za malipo ya stakabadhi, na elimu ya kifedha kwa wanachama wa ushirika ili kuongeza tija na matumizi sahihi ya mikopo.
Kwa upande mwingine, wadau wa sekta ya ushirika wameeleza kuwa kuanzishwa kwa benki hiyo ni hatua muhimu ya kuimarisha uchumi wa jamii na kuongeza ushirikishwaji wa wananchi kwenye mfumo wa kifedha rasmi.






