Breaking News

KADA WA CHADEMA LULU MAPUNGA AKATAA MAANDAMANO SIKU YA KURA

Na Mwandishi wetu - Mwanaharakati na muigizaji maarufu wa filamu nchini, Lulu Mapunda wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), ametoa wito kwa wanaharakati wenzake walioko nje ya nchi kusitisha mipango na juhudi za kuhamasisha maandamano katika kipindi hiki muhimu cha kuelekea Uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba 29.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Tanga, Lulu Mapunda alisisitiza kuwa jambo la msingi kwa sasa ni kuwapa nafasi Watanzania kushiriki kikamilifu katika zoezi la uchaguzi bila vuguvugu lolote la maandamano ambalo linaweza kusababisha taharuki na kuvuruga amani.

"Nawaomba wanaharakati wenzangu walioko nje ya nchi tusubiri uchaguzi upite kwanza. Tukishaona matokeo na hali ya kisiasa imetulia, ndipo tufanye maandamano ya amani kudai katiba mpya na masuala mengine ya msingi," alisisitiza Mapunda.

Lulu Mapunda alisisitiza kuwa uhai ni wa muhimu na kwamba athari za maandamano ya vurugu zitawaumiza wale waliobaki nchini.

"Tukivunjwa miguu, ni ndugu zetu watakaoshughulika na sisi, na tukiharibu nini tutafaidika nacho? Tutakao lia na kusaga meno ni sisi tuliopo hapa," alieleza, akiongeza kuwa wanaharakati wengi wa ndani wamekimbia, kiasi kwamba waliobaki nchini na wanaoposti Instagram ni wachache sana.

Aliongeza kuwa ni muhimu kukumbuka kuwa kila chama kinataka dola, na hata wale walio nje wangekuwa katika nafasi ya Serikali wangeona mapungufu kama hayo.

Muigizaji huyo aliwataka wanaharakati wote waliokimbilia nje ya nchi, mambo yakitulia baada ya uchaguzi, warudi nyumbani kwa ajili ya kupigania mabadiliko wakiwa nchini.

"Tukitaka kuandamana kwa amani, tuombe kibali; hata Polisi watatulinda, lakini tupishe uchaguzi upite kwanza kwani uchaguzi huo ulitangazwa awali," alisema na kuon geza kuwa polisi hawatakuwa tayari kuona vurugu zinakwamisha uchaguzi, na sisi hatutafaidika kwa vurugu.

Alimalizia kwa kukumbusha kuwa mabadiliko ya kweli hupatikana kwa njia ya kidemokrasia, na kwamba kuna ahadi za mabadiliko zimetolewa na kama wao wataona kusubiri utekelezaji utachukua muda basi ni vyema kuacha uchaguzi ufanyike na wan aharakati warejee nchini kufanya maandamano kwa utulivu