WAWILI WAREJESHA MILIONI 67 KUFUATIA UBADHIRIFU WA MILIONI 169 HALMASHAURI YA KIGAMBONI
Dar es salaam - Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Temeke imethibitisha kuwa watuhumiwa wawili wamekiri makosa na kurejesha jumla ya shilingi milioni 67 kufuatia tuhuma za ubadhirifu wa zaidi ya shilingi milioni 169 katika Halmashauri ya Manispaa ya Kigamboni.
Tuhuma hizo zilifuatia agizo la Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa, alilolitoa Oktoba 6, 2024, wakati wa ziara yake ya kikazi Kigamboni. Waziri Mkuu aliielekeza TAKUKURU Mkoa wa Temeke kushirikiana na Ofisi ya Taifa ya Mashtaka kuwachukulia hatua watumishi wa Halmashauri hiyo na baadhi ya watumishi wa Ofisi ya Rais – TAMISEMI waliotuhumiwa kuhusika na wizi na ubadhirifu wa fedha za serikali kiasi cha Shilingi 169,617,520/ maarufu kama fedha za bakaa.
Akizungumza mapema leo oktoba 27,2025 Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Temeke, Holle Makungu, amesema uchunguzi wa kina ulifanyika na kufikia Septemba 2, 2025, watuhumiwa 12 walifikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu mbele ya Mheshimiwa Hashim Makube.
Watuhumiwa hao walifikishwa mahakamani kwa makosa ya kuendesha genge la uhalifu, uchepushaji wa fedha, ubadhirifu, utakatishaji fedha na kuisababishia Serikali hasara — makosa yanayokiuka Sheria ya Uhujumu Uchumi Na. 200, Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Na. 329, na Sheria ya Utakatishaji Fedha Na. 423.
Miongoni mwa watuhumiwa hao ni watumishi wa Ofisi ya Rais – TAMISEMI, Halmashauri ya Kigamboni, na baadhi ya wafanyabiashara binafsi.
Katika maendeleo ya kesi hiyo, watuhumiwa wawili Juvenalis Babilas Mauna, aliyekuwa Mkuu wa Kitengo cha Usafi wa Mazingira Kigamboni, na Hamis Kashinje Manfred, Mkurugenzi wa Konya Investment Co. Ltd wamekiri makosa kupitia makubaliano maalum (plea bargain).
Kupitia makubaliano hayo, Mauna atarejesha Shilingi milioni 27 na kulipa faini ya Shilingi milioni 2, huku Manfred atarejesha Shilingi milioni 40 na kulipa faini ya Shilingi milioni 1.5.
Shauri dhidi ya watuhumiwa wengine 10 linaendelea, na kesi imepangwa kusikilizwa tena Novemba 6, 2025 kwa ajili ya hoja za awali.
Kesi hiyo inaendeshwa na mawakili wa Serikali Timoth Mmari na Patrick Mwita kutoka Ofisi ya Taifa ya Mashtaka, pamoja na Nickson Shayo kutoka TAKUKURU Mkoa wa Temeke.




