Breaking News

MIAKA MINNE YA RAIS SAMIA YALETA MAGEUZI MAKUBWA YA KIUCHUMI – KUFULILA

Na Mwandishi Wetu - Mkurugenzi wa Kituo cha Ubia kati Sekta ya Umma na Binafsi (PPPC), David Kafulila, miaka minne ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan imeleta mabadiliko ya kiuchumi nchini.

Kafulila amesema hayo leo mkoani Morogoro wakati wa Kongamano la Kitaaluma la Kujadili Utekelezaji wa Uchumi Jumuishi kufikia Dira ya Taifa 2050, lililoandaliwa na PPPC na Chuo Kikuu cha Waislamu Morogoro (MUM) na kushirikisha wataalamu na wananchi.

Amesema tathmini ya uchumi katika kipindi cha miaka minne imeonesha mabadiliko mengi kwenye sekta mbalimbali akitolea mfano sekta ya umwagiliaji ambayo awali hekta 540,000 ndizo zilikuwa zinazomwagiliwa ila hadi sasa hekta milioni moja zinanufaika na miradi ya umwagiliaji.

Kwenye sekta ya madini ilijulikana kuwa ni ya wachimbaji wakubwa na wageni, ila leo hii wachimbaji wadogo takribani 2600 wanamiliki leseni na kupelekea mchango wa wachimbaji wadogo pato la madini kuongezeka kutoka asilimia 20 wakati Rais Samia anaingia madarakani hadi kufikia asilimia 40 mwaka 2024.

"Rais Samia alipoingia madarakani alikuta msongo inayosafirisha umeme ulikuwa na kilomita 6000 kwa miaka 60 iliyopita lakini kipindi cha miaka minne ameongezeka kwa kilomita 2000 ambayo ni asilimia 30 ya kiasi ambacho kimetengenezwa kwa miaka 60, hiyo ndio maana halisi ya uchumi jumuishi,"

Mkurugenzi huyo amesema kazi hiyo ikitumia katika kipindi kijacho ni wazi utekelezaji wa Dira ya Taifa ya 2050 itafanikiwa kirahisi.
Kwa upande wa Makamu Mkuu wa Chuo cha MUM, Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali mstaafu (CAG) Profesa Mussa Assad, amesema ukuaji uchumi kwa miaka minne ya Rais Samia ni nzuri ambapo imefikia asilimia sita na mfumo wa bei ukiwa mzuri tofauti na kipindi cha nyuma.

Prof Assad amesema hata kwa vigezo vya kawaida uwezo wa watu kwa kipindi hiki ni mzuri kwa kuwa wanaishi maisha yao kwa ujumla wake, huku uchumi wa Tanzania ukiimarika kwa vigezo vya kiuchumi ukilinganisha na nchi za Kenya na Rwanda.

Akizungumzia kuhusu uchumi jumuishi, Prof Assad amesema, katika kipindi cha miaka 25 ijayo juhudi zinahitajika, ili kila mmoja aguswe na uchumi jumuishi.

Amesema juhudi zinahitajika kwa vijana wanaohitimu vyuo vikuu kupatiwa ujuzi ili waweze kushiriki kwenye uchumi jumuishi.

“Serikali na sekta binafsi ina wajibu wa kutoa elimu ya ujuzi kwa vijana tunaowatoa vyuoni ili waweze kuchangia kwenye dhana ya uchumi jumuishi," amesema.

Prof Assad amesema kwa maoni yake bado ukusanyaji wa takwimu unatumia mifumo ya kizamani akitolea mfano matumizi ya makaratasi wakati kwenye ukusanyaji wa mapato wanatumia mfumo wa kidigiti hivyo kuna haja kutumia mfumo huo kwenye kutoa taarifa.

Mchumi Dk Bravious Kahyoza, amesema tangu mwaka 2021 uwiano wa biashara na pato ghafi ulikuwa asilimia 27 na imefika asilimia 43 mpaka sasa ambayo inaonyesha fursa kuongezeka na watu wanafanya biashara.

Amesema sekta ya umma kwenye ajira katika kipindi cha miaka iliyopita ilikuwa haifanyi vizuri lakini katika kipindi cha miaka minne iliyopita imeweza kuajiri zaidi ya 400,000 na katika nchi zinazozunguka Tanzania hakuna nchi imeajiri kama ilivyofanya Tanzania.

“Katika kipindi cha miaka minne Tanzania imefanya vizuri kwenye sekta ya umma upande wa ajira ukilinganisha na Kenya watu 311,000,Uganda watu 196,000 na Rwanda 20,000,” amesema Dk Kahyoza.

Mhadhiri Chuo Kikuu Mzumbe ambaye Mtalaam wa PPP, Moshi Derefa, amesema uwekezaji duniani unafuata mfumo wa ubia kati ya sekta ya umma na binafsi, hivyo Tanzania tunapaswa kuweka nguvu huko.

“Tuna imani na tunaelewa wenzetu sekta binafsi wanakuwa wako mbele kidogo katika mazingira hayo kwa sababu unaposhirikisha sekta binafsi sio unashirikisha wadau kutoka ndani ya nchi lakini unashirikisha wadau au wawekezaji kutoka nje ya nchi ambazo zipo mbele zaidi kiteknolojia na kiujuzi kwa sekta mbalimbali,” amesema Moshi.