Breaking News

MKUDE ASEMA USALAMA UMETIMIZWA: WANANCHI WATAKIWA KUPIGA KURA KWA AMANI OKTOBA 29

Na Woinde Shizza, Arusha - Mamlaka za usalama katika Jiji la Arusha zimehakikisha maandalizi yote muhimu yamekamilika kuelekea uchaguzi mkuu wa Oktoba 29, 2025, ambapo zaidi ya wapiga kura 435,119 wanatarajiwa kushiriki katika zoezi hilo.

Akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Arusha, Mkuu wa Wilaya ya Arusha, Mhe. Joseph Mkude, amesema Serikali imejipanga kikamilifu kuhakikisha uchaguzi unafanyika kwa amani, utulivu na usalama wa hali ya juu.

“Tumehakikisha kila kitu kiko sawa. Hakutakuwa na maandamano yoyote zaidi ya yale ya kuelekea vituo vya kupigia kura, kufuatia agizo la Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, ambaye amehimiza wananchi kutumia haki yao ya kupiga kura kwa amani,” alisema Mkude.
Amesema hadi sasa hakuna chama cha siasa kilichowasilisha malalamiko kuhusu ukiukwaji wa taratibu za kampeni, na kwamba kampeni zote zimefanyika kwa ustaarabu, utii wa sheria na kuheshimiana.

Kwa mujibu wa Mkude, Jiji la Arusha lina jumla ya mitaa 154, na vituo vya kupigia kura vimepangwa kwa namna itakayowezesha kila mwananchi kutumia haki yake bila kutembea umbali mrefu.

“Tunataka kila mwananchi atumie haki yake ya kikatiba kwa mazingira salama Vyombo vyetu vya ulinzi na usalama vimejipanga ipasavyo kuhakikisha siku ya uchaguzi inabaki kuwa ya amani,” aliongeza.

Aidha, amewatoa hofu wafanyabiashara wanaotarajia kufungua maduka yao baada ya kupiga kura, akisema wana uhuru wa kufanya hivyo kwani amani itatawala siku nzima ya uchaguzi.

Hadi kufikia leo, vyama 16 kati ya 17 vilivyochukua fomu za kugombea vimefanikiwa kukamilisha mchakato wa kampeni katika Jiji la Arusha, huku chama kimoja kikishindwa kurejesha fomu zake.