Breaking News

VIJANA WAJITENGA NA MAANDAMANO, WAAPA KULINDA AMANI UCHAGUZI MKUU

Na Neema Nkumbi, Kahama - Vijana wilayani Kahama mkoani Shinyanga wamekataa kushiriki maandamano yaliyopangwa kufanyika siku ya uchaguzi mkuu Oktoba 29, na badala yake wameahidi kushiriki kikamilifu kupiga kura kwa amani, wakisisitiza umuhimu wa kudumisha utulivu na mshikamano wa kitaifa.

Makundi yaliyoshiriki kutoa tamko hilo ni pamoja na waendesha bodaboda na bajaji, wafanyabiashara wadogo maarufu kama machinga, mamalishe, walinzi wa jadi (Sungusungu) pamoja na wachimbaji wadogo wa madini.

Akizungumza katika mkutano uliofanyika viwanja vya Magereza, Mwenyekiti wa wachimbaji wadogo wa Mgodi wa Mwime Ilindi, Mohamed Juma, alisema vijana wa Kahama wamejipanga kushiriki uchaguzi kwa amani na hawako tayari kujiingiza kwenye maandamano yoyote.
“Siku ya uchaguzi tutasitisha shughuli za uzalishaji ili tukapige kura, ni haki yetu ya kikatiba hatutaki kuona uchaguzi unageuzwa uwanja wa vurugu, mwaka huu tumeamua kuwa mfano wa kuigwa kwa kutanguliza maslahi ya Taifa mbele,” amesema Juma.

Naye Mwenyekiti wa waendesha pikipiki na bajaji mkoa wa Shinyanga, Idisam Mapande, amesema vijana wanatambua kuwa wapo watu wanaohamasisha maandamano kupitia mitandao ya kijamii huku wakiwa nje ya nchi, hivyo hawana nia njema na Tanzania.

“Tumeamua hatutashiriki maandamano yoyote siku ya uchaguzi, Tunataka kuonyesha kwamba vijana wa nchi hii ni wazalendo na wanajali amani ya nchi yao, Maandamano yanaweza kutoa mwanya kwa watu wasiopenda amani kuchochea vurugu, jambo ambalo halitavumiliwa,” amesema Mapande.

Kwa upande wake, msemaji wa walinzi wa jadi (Sungusungu), Wiliamu Mondi, amesema wanatambua thamani ya amani ambayo ni tunu waliyoachiwa na waasisi wa Taifa, na hivyo wataendelea kuilinda kwa nguvu zote.

“Tunapenda kumhakikishia Mkuu wa Wilaya kuwa hakutakuwa na maandamano, Twendeni tukachague wagombea wetu kwa amani na tupinge uchochezi,” amesema Mondi.
Mzee wa jadi, Ukuku, amewasihi vijana kutoshiriki vitendo vyovyote vinavyoweza kuhatarisha amani ya nchi, akibainisha kuwa amani ndiyo imemwezesha kufika umri wa miaka 72.

“Amani iliyopo sasa nchini Tanzania ndiyo imeniwezesha kuishi miaka yote hii. Vijana mna ushawishi mkubwa, tumieni nguvu zenu kulinda amani ya nchi yetu,” amesisitiza Mzee Ukuku.

Mwenyekiti wa machinga wa Wilaya ya Kahama, Idrisa Kayombo, naye ameongeza kuwa vijana wa kundi hilo wamepata fursa nyingi kupitia mikopo na mazingira bora ya biashara chini ya serikali ya awamu ya sita, hivyo hawana sababu ya kushiriki maandamano.

“Samia ametuwezesha kupata mikopo na kufanya biashara bila usumbufu, Tutaenda kupiga kura kwa amani, siyo kuandamana,” amesema Idrisa.
Aidha, wachimbaji wadogo wameeleza kuwa serikali imewapa leseni na kupunguza changamoto walizokuwa wakikabiliana nazo, hivyo wanathamini maendeleo yaliyopatikana na hawako tayari kuyaharibu kwa kushiriki vurugu.

Mkuu wa Wilaya ya Kahama, Frank Nkinda, amewapongeza vijana hao kwa uamuzi wa busara, akisema serikali inathamini mchango wao katika kulinda amani na kuimarisha demokrasia.

“Nawapongeza sana vijana, bodaboda, machinga, wachimbaji wadogo na wazee wa jadi kwa hatua hii ya kuonyesha ukomavu wa kisiasa, Wilaya ya Kahama iko salama kabisa, na yeyote atakayevuruga amani atashughulikiwa kisheria,” amesema Nkinda.

Vijana hao wameahidi kushiriki uchaguzi huo kwa amani, huku wakisisitiza kuwa Tanzania haina utamaduni wa maandamano bali ni nchi inayojivunia umoja, upendo na utulivu.