Breaking News

WANU AAHIDI KULIPATIA SULUHISHO TATIZO LA MAJI MAKUNDUCHI

Mgombea Ubunge wa Jimbo la Makunduchi, Zanzibar kwa tiketi ya Chama cha Mapinduzi CCM Wanu Hafidh Ameir amewaahidi Wananchi wa jimbo hilo kuwa atasimamia utatuzi wa shida ya maji safi na salama ili Wananchi wafaidike na huduma hiyo muhimu kwa mahitaji ya kila siku.

Wanu ameeleza hayo wakati wa mkutano wa hadhara uliofanyika katika Viwanja vya Gereji Makunduchi Mkoa wa Kusini Unguja na kusisitiza kuwa kutakuwa na hatua za awali za uchimbaji wa visima ili kupunguza tatizo la maji wakati wakisubiria kufaidika na mradi mkubwa wa ujenzi wa matenki ya usambazaji wa maji katika Mkoa wote wa Kusini Unguja utaotekelezwa na Serikali chini ya Ilani ya Chama cha Mapinduzi.

Mgombea huyo wa Ubunge katika Jimbo la Makunduchi, Wanu Hafidh Ameir amesema Serikali itahakikisha inaleta miradi mikubwa ya Maji safi na salama utakaoweza kunufaisha maeneo yote ya Mkoa wa Kusini.

Akizungumzia Sekta ya Elimu amesema kwa Vijana watakaofanya vizuri kidato cha nne kwenda kidato cha tano pamoja kidato cha sita atawaezesha Wazazi na Walezi kwa kuwaondolea changamoto ya upatikanaji wa ada kwa Wanafunzi .

Amesema suala la uwezeshaji Wanawake kiuchumi atawaengezea kiwango ambacho wamekua wakichagiwa ili kuwainua kina Mama na kuwapa nafuu ya ugumu wa maisha.

Pia amefahamisha wanakwenda kufungua chuo cha ushoni kwa Vijana wa kike ambao watamaliza masomo yao ya Elimu ya juu.