CUF YATANGAZA FUNGA MAALUM YA KUMUOMBA MWENYEZI MUNGU KUHUSU DHULMA ZA UCHAGUZI
Dar es Salaam, Novemba 9, 2025 — Chama Cha Wananchi (CUF) kimetangaza kuwa kesho, Jumatatu Novemba 10, 2025, kutakuwa na ibada maalum ya funga kwa wanachama wake na wote wapenda haki na demokrasia, ikiwa ni hatua ya kumkabidhi Mwenyezi Mungu wale wote wanaodaiwa kufanya dhulma kabla, wakati na baada ya uchaguzi mkuu wa Oktoba 29, 2025.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Mkurugenzi wa Habari, Uenezi na Mahusiano na Umma wa CUF, Eng. Mohamed Ngulangwa, ibada hiyo inalenga kumlilia Mwenyezi Mungu ili kuomba haki na ulinzi dhidi ya nguvu za ukandamizaji.
Ngulangwa amesema CUF imeamua kuendeleza utamaduni wa viongozi waasisi wa harakati za ukombozi, akitaja mfano wa Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere ambaye aliwahi kufunga na wazee akiwemo Mzee Tambaza katika harakati za kupambana na utawala wa kikoloni.
“Tunawakumbusha wanachama wa CUF, wapenda demokrasia na haki, wapinga dhulma na ukandamizaji ndani na nje ya nchi, kushiriki katika funga hii kwa kuzingatia imani zao binafsi. Lengo kuu ni kuwashitaki kwa Mwenyezi Mungu wahusika wote wa dhulma, ikiwa ni pamoja na matukio ya mauaji yaliyotokea siku ya uchaguzi na baada yake,” amesema Ngulangwa.
CUF imeeleza kuwa funga hiyo ni mwendelezo wa tamko la chama hilo lililotolewa Novemba 5, 2025, likielekeza wanachama na wafuasi kuchukua hatua za kiroho katika kupinga ukandamizaji wa kisiasa.
“Hakuna mja mwenye nguvu inayoweza kupambana na nguvu ya Mola wake,” imesisitiza taarifa hiyo.




