HAYAKUWA MAANDAMANO YA AMANI, BALI UPORAJI NA KUHARIBU MALI
Hali ya usalama jijini Dar es Salaam ilivurugika vibaya baada ya kile kilichoanza kama "maandamano ya amani" kati ya Oktoba 29 na Novemba 1, 2025, kugeuka kuwa vurugu, uhalifu, na uharibifu mkubwa wa mali na miundombinu.
Taarifa za kiintelijensia zilizotolewa kabla ya Oktoba 29, 2025, kuhusu uwezekano wa maandamano hayo kugeuka ghasia zimethibitishwa kuwa sahihi.
Ndani ya muda wa dakika 40 tangu kuanza kwa matukio hayo, taarifa zilionyesha kuwa hasara ilianza kutokea:
Vituo viwili vya Mabasi Yaendayo Haraka (BRT) vilichomwa moto,Basi moja la mwendokasi liliharibiwa huku vituo vya mafuta na maduka ya wananchi yalichomwa moto au kuharibiwa vibaya.
Vurugu Zashika Kasi, Vijana wa Mitaani Wahusishwa
Siku iliyofuata, hali kama hiyo ilirudiwa katika mitaa kadhaa, ikiwemo Mpiji Magoe, ambako maduka yalivunjwa na vibaka wakapora mali za wananchi. Inadaiwa baadhi ya wananchi walijeruhiwa walipojaribu kulinda mali zao.
Akizungumza kwa masharti ya kutotajwa jina, mkazi mmoja wa eneo la Mpiji Magoe alieleza kushangazwa na wahalifu hao.
“Huku mtaani kwetu imetushangaza sana kwani waliohusika ni vijana wa hapa hapa mtaani wanajiita wazawa, pamoja na kijana mmoja wa ulinzi shirikishi. Wamevunja maduka ya watu na kuiba simu, nguo na vitu vingine wakisingizia maandamano.”
Hasira za wananchi ziliongezeka baada ya kudhihirika wazi kuwa baadhi ya watuhumiwa walitumia jina la maandamano kufanya uporaji. Kijana mmoja aliyekuwa kiongozi wa ulinzi shirikishi alikamatwa akiwa na simu zaidi ya 60, madela, na vitu vingine alivyopora.
Mkazi mwingine alieleza ghadhabu zao: “Ni ajabu kwamba mtu tuliyemtegemea kama kiongozi wa ulinzi shirikishi, kumbe ni mporaji na mharibifu wa mali. Sina huruma na watu wa aina hii, waadhibiwe tu.”
Maandamano ya Giza
Mashuhuda walibainisha kuwa vurugu hazikuwa za mchana, na badala yake zilianza jioni, muda ambao kulikuwa na amri ya kutotembea baada ya saa 12 jioni (curfew).
“Ilitushangaza, maana kama ni maandamano ya amani si yanafanyika mchana? Lakini vurugu zilianza jioni, muda ambao kulikuwa na amri ya kutotembea barabarani. Ni wazi hawa walikuwa wahalifu waliotumia jina la maandamano kufanya uhalifu,” alisema mkazi mwingine.
Wito wa Viongozi na Wananchi
Baadhi ya wahalifu walitambuliwa na kukamatwa kwa ushirikiano wa wananchi na Jeshi la Polisi. Mmoja wa viongozi wa Serikali ya Mtaa ametoa shukrani kwa wananchi kwa ushirikiano wao katika kuwafichua waharibifu, na akatoa wito kwa walioibiwa kufika ofisini kwake kuchukua mali zao zilizookolewa.
Kiongozi huyo alisisitiza kuwa “usalama wa jamii ni jukumu la kila mmoja wetu” na kuwataka wananchi kuendelea kushirikiana na Vyombo vya Ulinzi na Usalama.
Wakazi wa maeneo yaliyoathirika wametoa wito kwa jamii kutojiingiza tena kwenye maandamano yasiyo na uhalisia wa amani, wakisema matukio hayo yamethibitisha wazi kuwa maandamano mara nyingi hutumiwa na wahalifu kutekeleza vitendo vya uporaji, uharibifu wa mali, na kuvuruga utulivu wa Taifa.




