Breaking News

MAKAMU WA PILI WA RAIS WA ZANZIBAR AZINDUA MAONESHO YA 12 YA KIMATAIFA YA BIASHARA ZITF

Zanzibar - Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Mheshimiwa Hemed Suleiman Abdulla, amezindua rasmi Maonesho ya 12 ya Kimataifa ya Biashara Zanzibar (ZITF) katika viwanja vya Nyamanzi, Januari 7, 2026.

Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Mheshimiwa Abdulla amesema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inaendelea kuweka mazingira rafiki kwa wawekezaji na wafanyabiashara ili kuchochea ukuaji wa uchumi. Amesisitiza kuwa ushiriki wa sekta binafsi ni nguzo muhimu katika kufanikisha maendeleo endelevu ya taifa, huku akihimiza wadau mbalimbali kutumia fursa zinazopatikana kupitia maonesho hayo kupanua mitandao ya biashara na uwekezaji.
Katika maonesho hayo, Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) iliwakilishwa na Mkurugenzi wa TMA Ofisi ya Zanzibar, Bw. Masoud Makame Faki. Bw. Faki aliwahimiza wananchi na wadau wa maendeleo kutembelea banda la TMA ili kupata elimu ya sayansi ya hali ya hewa, hususan katika kipindi hiki ambacho dunia inakabiliwa na changamoto za mabadiliko ya tabianchi.

Alieleza kuwa mabadiliko ya mifumo ya hali ya hewa yamekuwa yakijitokeza mara kwa mara na kusababisha athari katika sekta mbalimbali za kiuchumi na kijamii. Hivyo, alisisitiza umuhimu wa matumizi sahihi ya taarifa za hali ya hewa kama suluhisho mbadala la kukuza uchumi na biashara katika sekta tofauti zikiwemo kilimo, uvuvi, viwanda, nishati, ujenzi na mawasiliano.

Maonesho ya ZITF yanatarajiwa kuwakutanisha wafanyabiashara, wawekezaji na taasisi mbalimbali kutoka ndani na nje ya nchi, yakiwa na lengo la kuimarisha biashara, uwekezaji na ushirikiano wa kiuchumi.