Breaking News

WAZIRI KOMBO: ELIMU MLIYOIPATA IWE CHACHU KWA MAENDELEO YA TAIFA

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Mahmoud Thabit Kombo (Mb.) amewatunuku vyeti wahitimu 900 wa ngazi na fani mbalimbali za masomo katika Kituo cha Uhusiano wa Kimataifa cha Dkt. Salim Ahmed Salim (SAS-CFR) katika mahafali ya 28 ya kituo hicho yaliyofanyika katika ukumbi wa Diamond Jubilee, jijini Dar es Salaam.

Akihutubia wakati wa mahafali hayo, Waziri Kombo amewataka wahitimu kutumia elimu na maarifa waliyoyapata kuwa chachu ya mabadiliko chanya kwa Taifa, kwa kujikita katika ubunifu, uadilifu na uzalendo.

Mhe. Kombo ameeleza kuwa elimu ni nyenzo muhimu ya kutatua changamoto zinazolikabili Taifa na maisha binafsi ya wahitimu na kuwaasa kuangalia fursa za kujiajiri kwa kutumia elimu na ujuzi walioupata katika kipindi chote cha elimu yao.
“Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi mahiri wa Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, imeelekeza kila Halmashauri itenge bajeti kwa ajili ya mikopo ya vijana, wanawake na makundi maalumu kwa shughuli za ujasiriamali ili kukabiliana na tatizo la ajira. Nawasihi kuchangamkia fursa hizo. Pia kwa wale mliopo kazini nawasihi kutumia elimu mliyoipata kwa kuwa wabunifu na kutatua changamoto za wananchi kupitia kazi zenu,” ameeleza Mhe. Kombo.

Naye, Mwenyekiti wa Baraza la uongozi la SAS-CFR Balozi Ramadhan Muombwa Mwinyi ameiomba Serikali kupitia Wizara kuwafikiria wahitimu hao wa masuala ya kimataifa pale inapotokea fursa zinazohitaji wahitimu wa fani zitolewazo na SAS-CFR.

Wahitimu 900 wametunukiwa vyeti katika fani za Uhusiano wa Kimataifa na Diplomasia; Menejimenti ya Uhusiano wa Kimataifa; Amani na Menejimenti ya Migogoro; Diplomasia ya Uchumi na Utawala wa Mikakati.