NABII MKUU PROF. GEORDAVIE ATUNUKIWA CHEO CHA UPROFESSOR
Na Woinde Shizza, Arusha - Dunia ya elimu na dini imeshuhudia tukio la kihistoria baada ya Nabii Mkuu Prof. Geordavie, ambaye pia ni Balozi wa Amani, kutunukiwa cheo cha Uprofesa wa Kitaaluma katika hafla maalum iliyofanyika katika Nyumba ya Matamko Ngurumo ya Upako, Kisongo mkoani Arusha.
Akizungumza kama mgeni rasmi kwa niaba ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais – Kazi Maalumu Ikulu, Prof. Palamagamba Kabudi, alisema kuwa cheo hicho si heshima ya kawaida bali ni uthibitisho wa mchango mkubwa wa Prof. Geordavie katika nyanja za elimu, uongozi wa kiroho na amani.
Prof. Kabudi alisisitiza umuhimu wa elimu kwa viongozi wa dini na jamii, akibainisha kuwa elimu ni msingi wa uongozi bora na chachu ya heshima katika jamii.
“Elimu humwezesha kiongozi kuelewa kwa kina masuala ya kidini na kijamii, kushughulikia changamoto za kisasa na kuwa mfano bora kwa jamii,” alisema Prof. Kabudi.
Akifafanua faida za elimu ya juu kwa viongozi wa dini, Prof. Kabudi alisema elimu huongeza uelewa wa kina wa neno la Mungu, huimarisha uwezo wa kukabiliana na maendeleo ya teknolojia na sayansi, huchangia kudumisha amani na mshikamano wa kijamii, pamoja na kuimarisha ushirikiano na wataalamu kutoka nyanja mbalimbali.
“Viongozi walioelimika wana uwezo wa kushirikiana na wadau mbalimbali bila kupoteza misingi ya imani na maadili,” aliongeza.
Katika hotuba yake, Prof. Kabudi pia alielezea mafanikio ya Prof. Geordavie, akisema amesoma vitabu vyake vilivyozinduliwa vinavyojikita katika diplomasia ya kimataifa na ushirikiano wa kimkakati wa Afrika, akivitaja kuwa ni mchango muhimu katika kukuza uongozi wa amani barani Afrika.
Kwa upande wake, Prof. Geordavie alikumbusha tuzo ya kimataifa ya amani aliyopokea, International Law Mayor of Peace Award, iliyotolewa na International Association of World Peace Advocates kwa kushirikiana na Association of the United Nations, jijini Nairobi, Kenya, tarehe 7 Januari 2025.
Alisisitiza dhamira yake ya kuendelea kujenga jamii yenye maadili, mshikamano na heshima kwa misingi ya amani na haki, huku akibainisha nafasi muhimu ya Afrika katika ushirikiano wa kimataifa.
Kwa ujumla, hafla hiyo imeonesha wazi umuhimu wa elimu, uongozi wenye maadili na mshikamano wa kimataifa katika kuleta maendeleo endelevu na amani katika jamii, na kuweka mfano wa viongozi wanaoweza kuunganisha maarifa ya kitaaluma na maadili ya kiroho kwa manufaa ya jamii pana.









