MBETO: TUMEMPOTEZA KIONGOZI KIOO CHA UPATANISHI
Na Mwandishi Wetu, Zanzibar - Chama Cha Mapinduzi kimemtaja aliyekuwa Waziri wake wa Nchi ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu, William Vangimembe Lukuvi, amekuwa kamusi iliosaidia kufafanua na kuelekeza kila alipohitajika kutoa ushauri katika mambo ya msingi.
CCM kimesema kiongozi huyo alikuwa kiungo na kiraka kilichoziba lolote katika nyakati zote ngumu aidha kwa masuala ya Kisiasa,kiutendaji na Kiutawala.
Katibu wa Kamati Maalum ya NEC Zanzibar Idara ya Itikadi,Uenezi na Mafunzo , Khamis Mbeto Khamis , ameeleza hayo kwa masikitiko, huzuni na fazaa kufuatia kifo cha Mwanasiasa huyo.
Mbeto alisema Tanzania imepoteza kiongozi wake madhubuti, jasiri , mzalendo na mshauri muhimu wa vipindi vyote katika maisha ya kiongozi huyo.
Alisema kuna mambo muhimu sana yatakayofanya Lukuvi azidi kukumbukwa na jamii katika utumishi wake kwa kuwa kioo kilichoakisi tija na utatuzi wa changamoto katika Siasa, Utumishi na Utawala
"Kuwa kwake katika Utumishi kwa Muda Mrefu kulikuzia johari ya maarifa yake ,uzoefu na upeo wa kupambanua mambo kila alipohitajika kwa niaba ya nchi yake" Alisema Mbeto
Aidha Katibu huyo Mwenezi alisema licha ya kuwa Mbunge pekee aliyekaa Bungeni kwa muda mrefu zaidi akitumikia Jimbo la Isimani Mkoani Iringa kwa miaka 30 tangu 1995 .
Mbeto alisema Lukuvi alikuwa Kiongozi jasiri, shupavu ,mtiifu na muaminifu kwa nyakati zote.
"Lukuvi ameondoka duniani akiwa ameshiba siha ya uaminifu na uzalendo , Mchapakazi asiyechoka kutumikia nchi na chama chake" Alisisitiza.
Mbeto akiutaja Ujasiri wake , alisema alikuwa mahiri wa kupatanisha na kusuluhisha tofauti za kimtazamo zinapochomoza ndani ya Serikali na chama na kuyaweka mambo sawa.
"Hakuwahi kutajwa kama kiongozi shabiki au shawishi wa makundi ya hasama. Hakuwa kiongozi aliyeingilika kirahisi au kumtoa katika reli ya msimamo wake, kwa chama na Taifa lake" Alisema Mbeto kwa huzuni.




