WAZAZI WA VIJANA WALIOREJESHWA KUTOKA IRAN WAWASILISHA SHUKRAN ZAO WIZARA YA MAMBO YA NJE
Dar es Salaam - Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Said Shaib Mussa, amekutana na Balozi wa Shirikisho la Khoja Shia Ithna-Asheri Jamaats ya Afrika, Aunali Khalfan, pamoja na familia za wanachama walioathirika na mgogoro wa Iran.
Mkutano huo ulifanyika katika ofisi ndogo za Wizara jijini Dar es Salaam, ukilenga kujadili hatua zilizochukuliwa na serikali katika kuwaokoa na kuwarejesha nyumbani wanafunzi waliokuwa katika maeneo ya machafuko.
Akizungumza katika kikao hicho, Balozi Mussa alitoa shukrani kwa wawakilishi hao kwa kufika wizarani na kusisitiza dhamira ya serikali ya kuendelea kuwalinda na kuwasaidia raia wa Tanzania popote walipo, hasa nyakati za dharura.
Kwa upande wake, Alhaj Khalfan aliishukuru Serikali ya Tanzania kwa juhudi zake za kuratibu zoezi la kuwaokoa na kuwarejesha wanafunzi waliokuwa wamekwama nchini Iran kufuatia hali ya usalama.
Naye mzazi wa mmoja wa wanafunzi waliorejea, Bi Zia, alieleza hofu waliyoipata wazazi wakati wa mgogoro huo. Alipongeza juhudi za Wizara pamoja na Idara ya Mashariki ya Kati chini ya Abdallah Kilima kwa msaada uliowezesha kurejea salama kwa vijana hao.
Aidha, aliomba serikali kuendelea kutoa msaada wa haraka kwa raia wa Tanzania watakaokumbwa na majanga au migogoro inayoweza kuhatarisha maisha yao.
Kwa pamoja, wawakilishi hao walisisitiza umuhimu wa kuendeleza ushirikiano kati ya serikali na taasisi za kijamii, wakilitaja zoezi hilo kuwa mfano wa diplomasia inayojali watu na yenye mwitikio wa haraka.






