Breaking News

MFUMO WA EWURA e-SERVICES KUANZA KAZI LEO 02 Machi.

Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) imetangaza kuanza rasmi kwa matumizi ya mfumo wake mpya wa kidijitali unaojulikana kama EWURA e-Service, utakaotumika kwa maombi yote ya vibali na leseni kuanzia tarehe 2 Machi 2026.

Akitoa taarifa hiyo, EWURA imeeleza kuwa uboreshaji huo ni sehemu ya jitihada za kuongeza ufanisi, uwazi na kurahisisha upatikanaji wa huduma kwa wateja wake. Kupitia mfumo wa EWURA e-Service, waombaji watawasilisha maombi ya vibali vya ujenzi na leseni kwa njia ya mtandao, hatua inayotarajiwa kupunguza muda na gharama za utoaji wa huduma.

Aidha, EWURA imefafanua kuwa kuanzia tarehe 2 Machi 2026, mfumo wa zamani wa LOIS hautatumika tena kwa ajili ya maombi ya vibali vya ujenzi na leseni. Hata hivyo, mfumo wa LOIS utaendelea kutumika kwa ajili ya kupokea na kushughulikia malalamiko ya wateja.

Mamlaka imewahimiza wateja na wadau wote kujipanga kutumia mfumo huo mpya mara tu utakapoanza kutumika rasmi.
Kwa mawasiliano zaidi, wateja wanaweza kupiga simu bure namba 0800 110 030 au kutuma barua pepe kupitia info@ewura.go.tz.