Breaking News

RC CHALAMILA ATOA WIKI MOJA KWA WATUHUMIWA WA UPORAJI WA ARDHI

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila, ametoa wiki moja kwa watu wote wanaodaiwa kujihusisha na vitendo vya utapeli na unyang’anyi wa ardhi kujitokeza na kurejesha mali walizozipora kabla ya kuchukuliwa hatua za kisheria.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, amesema uchunguzi wa kina umebaini kuwepo kwa makundi yanayoshirikiana na baadhi ya watu ndani na nje ya mifumo ya kiutendaji kufanya vitendo hivyo.

Amesema hadi sasa ardhi zisizopungua 19 tayari zimerudishwa kwa hiari na wahusika, ambao wamepewa msamaha baada ya kurejesha mali hizo.

“Tumewapa nafasi ya kujirekebisha. Wale waliojitokeza na kurejesha ardhi zao kwa ridhaa yao tumewaonea huruma,” alisema.

Kwa mujibu wa Chalamila, waathirika wakubwa wa matukio hayo ni wajane, warithi na familia zilizopoteza wazazi au walezi, ambao mali zao zimekuwa zikinyakuliwa kwa hila.

Utapeli wa ‘Showroom’ za Magari
Mbali na migogoro ya ardhi, alibainisha kuwepo kwa mtandao wa utapeli katika showroom za magari, ambapo wananchi hulipia magari wakiamini yapo bandarini, ilhali baadhi hayapo kabisa au yapo bandarini yakiwa na madeni yasiyolipwa.

Ameonya kuwa hatua kali zitachukuliwa kwa wote watakaobainika kuhusika.

Mikopo Umiza Yachunguzwa Chalamila pia alizungumzia mikopo umiza, akisema baadhi ya wakopeshaji huwafanya wakopaji kusaini mikataba ya mkopo sambamba na mikataba ya kuuza ardhi, hali inayosababisha kupoteza mali wanaposhindwa kulipa.

“Huu ni unyang’anyi wa aina nyingine unaofanyika kwa njia ya hadaa,” alisema.

Wiki Moja kwa Watuhumiwa

Amesema tayari majina ya baadhi ya wanaodaiwa kuhusika yamebainika na kuwataka warejeshe ardhi hizo ndani ya wiki moja.

“Wasipofanya hivyo, hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi yao,” alisisitiza.

Amewashukuru Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Leonard Akwilapo, pamoja na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), vyombo vya ulinzi na usalama na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa ushirikiano wao.

Kesi ya Mbagala

Akizungumzia mgogoro wa ardhi uliopo Mbagala, alisema kuna mtu aliyeingia kwa makubaliano ya upangaji wa muda mfupi lakini baadaye akaghushi nyaraka kuonyesha ana haki ya muda mrefu na kuanza kudai umiliki.

Aidha, alimtaja mpangaji aliyeshindwa kulipa kodi akidai kuwepo kwa mgogoro wa pande mbili, akimtaka ajitokeze ndani ya wiki moja, vinginevyo hatua za kisheria ikiwemo mashitaka ya utakatishaji fedha zitachukuliwa.
Maeneo Yanayoongoza kwa Migogoro

Ametaja maeneo yanayoongoza kwa migogoro ya ardhi kuwa ni Kigamboni, Kinondoni na Ilala, akiwataka wananchi wenye malalamiko kufika ofisini kwake wakiwa na ushahidi kamili ifikapo Machi 9.

Ametangaza kuanza ziara ya mguu kwa mguu katika maeneo yenye migogoro, akianzia Ilala, huku akisisitiza kuwa serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan imelenga kuhakikisha kila mwananchi anapata haki bila upendeleo.

“Waliolia kwa muda mrefu waje na ushahidi. Serikali iko tayari kusimamia haki,” amesema.