VIJANA WATAKIWA KULINDA AMANI NA KUCHANGAMKIA FURSA ZA KIUCHUMI
Na Mwandishi Wetu - Vijana nchini wametakiwa kuendelea kulinda amani, umoja na mshikamano uliopo, huku wakiepuka vitendo vya uvunjifu wa amani na badala yake kujikita katika kufanya kazi kwa bidii ili kujiletea maendeleo.
Wito huo umetolewa na mjasiriamali wa ufundi wa fenicha, Bw. Jerry Mushi, katika mahojiano maalum, akisisitiza kuwa amani na utulivu ni msingi muhimu unaowawezesha vijana kutimiza ndoto na maono yao.
Amesema kila kijana ana wajibu wa kulinda na kudumisha mshikamano wa kitaifa kwani hali hiyo huchangia maendeleo ya mtu mmoja mmoja, familia na Taifa kwa ujumla.
“Uwepo wa amani ni nyenzo muhimu katika kufikia matarajio yetu. Bila amani, utulivu na mshikamano wa jamii, itakuwa vigumu kwa sekta binafsi na wananchi kwa ujumla kujiendeleza kiuchumi na kijamii,” alisema Bw. Mushi.
Aliongeza kuwa kukosekana kwa utulivu kunadhoofisha juhudi za maendeleo, hivyo kuwataka vijana kuthamini na kulinda hali ya amani iliyopo nchini.
“Hatutaweza kufanya kazi kama nchi haina utulivu. Niwaombe vijana wenzangu tuilinde amani, utulivu na mshikamano wetu kwa gharama yoyote, kwani ndoto zetu zitatimia iwapo tutakuwa na mazingira ya amani,” alisisitiza.
Aidha, aliwahimiza vijana kuchangamkia fursa mbalimbali za kiuchumi zilizopo nchini kwa kujikita katika shughuli za uzalishaji mali, akibainisha kuwa mazingira ya amani yaliyopo yanatoa nafasi kubwa ya kufanikiwa kiuchumi.
Bw. Mushi alihitimisha kwa kusisitiza kuwa mafanikio ya vijana na Taifa kwa ujumla yanategemea juhudi za pamoja katika kulinda amani na kutumia ipasavyo fursa zilizopo.




